Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA NA KUMTISHIA KUMUUA MTOTO WAKE WA KUZAA MWENYEWE



Na Walter Mguluchuma -Katavi .

Mwanaume aliyefahamika kwa jina la Agustino Mikese Mkazi wa Kijiji cha Isinde Kata ya Mtapenda Halmashauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kumbaka na kumtishia kumuua mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 16 (jina limehifadhiwa).

Mtuhumiwa huyo amekamatwa Januari 6,2023 baada ya mtoto huyo kuona vitendo hivyo vya kubakwa na baba yake kuwa vimemzidia .

Mtoto huyo baada ya kuona baba yake amekuwa akimfanyia vitendo hivyo vya kikatili mara kwa mara na kumtishia kumuua aliamua kwenda kutoaa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Isinde .

Baada ya tukio hilo kufikishwa katika uongozi wa Serikali ya Kijiji ndipo walipotoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.

Polisi baada ya kuwa wamepokea taarifa hizo walianza kufuatilia na ndipo hapo Januari 6 mwaka huu walipomkamata mtuhumiwa huyo akiwa kijijini hapo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Isinde Hamis Rashid Mbogo amesema kuwa kabla ya mtuhumiwa huyo kukamatwa ndugu wa mtuhumiwa huyo walikuwa wameshasikia tuhuma za ndugu yao kuwa na tabia ya kumfanyia ukatili huo mtoto wake wa kumzaa mwenyewe.

Amesema mtoto huyo alikuwa akiishi nyumbani kwao akiwa na wazazi wake wote wawili ambapo mama yake mzazi kwa sasa ni mjamzito.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Ally Hamad Makame amesema kuwa mtuhumiwa huyo bado anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusiana na tuhuma hizo.

Amesema wamefanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo kwa kumfanyia mtoto huyo vipimo vya kidaktari.

Kamanda Makame ameeleza kuwa mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa Mahakamani wakati wowote ili akajibu tuhuma zinazomkabili .


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com