Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabambasi kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Bakari Hamis
**
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wakati wanaharakati wa haki za wanawake na watoto wakiendelea kupaza sauti jamii kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabambasi kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Bakari Hamis amesema ni vyema jamii ikajikita katika kuzuia ukatili badala ya kujitokeza baada ya tukio kufanyika.
Mwenyekiti huyo wa Mtaa wa Mabambasi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 16,2023 wakati akitoa neno kwenye msiba wa mkazi wa mtaa huo Bi. Asia Mdadila (85) aliyefariki dunia jana Jumapili baada ya kuanguka Jumamosi na kulazwa hospitali ambapo mazishi yamefanyika leo mchana.
Khamis amesema bado matukio ya ukatili dhidi ya wanawake yanaendelea katika jamii ikiwemo wanandoa kuuana jambo ambalo amesema mwarobaini wake ni jamii kuzuia vitendo hivyo wanapoona dalili mbaya kabla havijatokea.
“Wananchi acheni kunyamaza mnaposhuhudia matukio ya ukatili,msichukulie poa mambo haya. Utakuta mke na mme wanapigana kila siku lakini nyinyi mnanyamaza tu, matokeo yake mauaji yakitokea mnaanza kusema hawa walikuwa wanapigana kila mara, ama tuliwaona wanagombana tukaona tusiingilie mambo ya watu, au tulisikia tu mtu anapiga kelele”,amesema Khamis.
“Ndugu zangu naomba tuishi kwa amani na utulivu, tusinyamazie tunapoona dalili za ukatili wa kijinsia. Nawasisitiza sana sana kuzingatia uvumilivu na kufuata sheria. Unapokuwa umepatwa na jambo lolote lile vipo vyombo mbalimbali vya kutatua mambo kuanzia katika ofisi za serikali za mitaa,kata, wilaya,mkoa na kitaifa.
“Hakuna sababu za raia yeyote kujichukulia sheria mkononi, mnakumbushwa sana kufuata sheria zilizowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria na miongozo ya dini hairuhusu mtu kuua”,ameongeza Khamis.
Khamis amesema uongozi wa Mtaa huo unaendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia mikusanyiko mbalimbali kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Social Plugin