Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu ,Cheick Sangare (kushoto) pamoja na Katibu mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini na Kazi za Ujenzi (TAMICO) Paternus Rwechungura (katikati) wakisaini Makubaliano ya Mkataba wa Hali bora kazini katika hafla iliyofanyika katika mgodi wa Bulyanhulu,(kulia) ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga akiongea wakati wa hafla hiyo
Wafanyakazi wa Barrick Bulyanhulu wakifuatilia matukio wakati wa hafla hiyo
Picha ya pamoja ya Viongozi wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu na wafanyakazi pamoja na Katibu mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini na Kazi za Ujenzi (TAMICO) Paternus Rwechungura, Mkuu wa wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga, na kamishna wa kazi Msaidizi, Andrew Mwalwisi kutoka ofisi ya waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu baada ya hafla ya kusaini Makubaliano ya Mkataba wa Hali bora kazini katika hafla iliyofanyika katika mgodi wa Bulyanhulu.
Mgodi wa dhahabu wa Barrick Bulyanhulu, uliopo katika halmashauri ya Msalala, Wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga umesaini Makubaliano ya hiari ya Hali Bora kazini na wafanyakazi wake.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika katika mgodi wa Barrick Bulyanhulu na kushuhudiwa na Mkuu wa wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga, Festo Kiswaga, ambapo upande wa mgodi uliwasilishwa na Meneja Mkuu wa Mgodi huo Cheick Sangare na kwa upande wa wafanyakazi Katibu mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini na Kazi za Ujenzi (TAMICO), Paternus Rwechungura.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Madini, Nishati na Ujenzi, (TAMICO) Bw. Rwechungura, amesema makubaliano haya yamefanikiwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya menejimenti ya mgodi na TAMICO.
Amesema makubaliano haya yamelenga kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa Barrick kwa kuwapa stahiki zao, mafao baada ya kustaafu kazi na fedha za motisha kwa ajili ya kusomesha watoto wa wafanyakazi.
Ameeleza kuwa, Makubaliano ya Mkataba wa Hali bora ni hatua ya utekelezaji wa Sheria za kazi hususani Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo uweka mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kitaasisi baina Wafanyakazi na Waajiri kwa lengo la kuboresha mazingira bora ya kazi, maslahi ya Wafanyakazi na kuleta tija mahala pa kazi.
Rwechungura, amesema amefurahishwa kuona uongozi wa mgodi umeona umuhimu wa makubaliano haya ambayo kwa kiasi kikubwa yataongeza morali ya kazi, kutokana na kukuza mahusiano mema kazini.
Meneja Mkuu wa Mgodi huo Cheick Sangare, amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni kielelezo tosha cha Mgodi huo kwenda kuyafanyia kazi makubaliano hayo, kwa mujibu wa Sheria huku akiwataka wafanyakazi kutimiza wajibu wao.
"Tumekubaliana Na pande zote mbili kuboresha maslahi jambo ambalo sisi tutazingatia Hilo na kutoka kwenu wafanyakazi tunategemea kuona mnaongeza juhudi na ubunifu katika kufanya kazi ili tupate wote manufaa katika kuongeza uzalishaji", amesema Sangare.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga, ameupongeza Mgodi huo kwa kuridhia makubaliano hayo ambayo pia yataongeza maslahi ya Wafanyakazi na kuongeza pato la Serikali kupitia kodi ya mshahara inayotozwa na Mamlaka ya mapato nchini TRA.
Kiswaga, ametumia nafasi hiyo kuwataka wafanyakazi kuongeza juhudi katika uzalishaji wa madini ili kupandisha pato la mgodi kutokana na kuuza dhahabu nyingi katika soko la Dunia la madini hayo.
Hafla hiyo pia imeshuhudiwa na Kamishna wa kazi Msaidizi, Andrew Mwalwisi kutoka ofisi ya waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu ambaye licha kupongeza kufikiwa kwa Mkataba huo, amewataka waajiri wote nchini kuzingatia kulipa viwango vipya vya mishahara ikiwemo kima cha chini cha mshahara kilichotangazwa na serikali.
Amesema kima cha chini cha mshahara kimepanda lakini kumekuwa na tabia ya baadhi ya waajiri katika kampuni binafsi na umma nchini kupuuza takwa la kisheria la kulipa viwango vilivyoelekezwa na serikali.
Mwenyekiti wa tawi la TAMICO mgodi wa Bulyanhulu, Maghembe Malimi, amepongeza hatua hiyo na kuahidi kuwa wafanyakazi wako tayari kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza uzalishaji wa dhahabu katika mgodi huo.