Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni! Mrembo Primrose Mwangi anatuhumiwa kushirikiana na genge la wahalifu kuchezea mfumo na kuiba kiasi kikubwa cha pesa zipatazo zaidi ya bilioni 280 za Kitanzania.
Mwangi ambaye ni raia wa Kenya anadaiwa kutekeleza uhalifu huo nchini Zimbabwe akihusishwa na udukuzi katika mifumo ya shirika moja la serikali nchini humo liitwalo Zimbabwe Manpower Development Fund (Zimdef) na kuhamisha Dola za Kimarekani milioni 120 (zaidi ya shilingi bilioni 280 za Kitanzania) kutoka kutoka kwenye akaunti hiyo hadi kwenye akaunti yake ya kibinafsi ya benki.
Akiwa mbele ya Mahakama ya Harare nchini Zimbabwe, Mwangi ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya usafiri alishtakiwa kwa kushirikiana na washukiwa wengine kudukua mifumo ya kompyuta ya Zimdef na kuhamisha kiasi kikubwa cha pesa hadi kwenye akaunti zao. Mwangi na wenzake wanadaiwa kutekeleza uhalifu huo mwezi Desemba, mwaka jana.
Vyombo vya habari vya Zimbabwe vimeripoti kuwa Mwangi na washirika wake walihamisha kiasi tofauti cha pesa kutoka akaunti ya Zimdef kwenda kwenye akaunti ya Benki ya Steward ya Maffikett Trading, akaunti ya Atrier Engineering CBZ, akaunti ya Tavaka Holding NBS na akaunti ya Newplaces Limited ya NBS.Mtoa taarifa alifichua uhalifu huo kupitia barua pepe mnamo Desemba 28, mwaka jana na hatua ikachukuliwa.
Iwapo watapatikana na hatia, Mwangi na washirika wake ambao hawajulikani waliko kwa sasa wanaweza kukabiliwa na adhabu kali sana. Polisi nchini humo wanaendelea kuwasaka wenzake Mwangi.
Mwangi pia anakabiliwa na mashtaka mengine ya kukiuka sheria za visa kwa kufanya biashara nchini Zimbabwe ilihali yuko nchini humo kama mtalii.
STORI NA SIAEL PAUL