Hali isiyokuwa ya kawaida imeshuhudiwa mjini Hong Kong, China baada ya mfanyakazi wa kichinjio kufariki dunia alipokuwa akijaribu kuchinja nguruwe.
Kwa mujibu wa ripoti ya BBC ikinukuu CNN, mchinjaji huyo mwenye umri wa miaka 61, alikumbana na mauti yake alipomshtua nguruwe kwa umeme ili kumchinja. Lakini mnyama huyo alipata fahamu haraka, akajitengua na kumshambulia mtu huyo.
Kisha mchinjaji huyo alianguka kwenye kisu cha sentimita 40 na kujeruhiwa vibaya kwenye mguu wake wa kushoto.
Marehemu alipatikana na mwenzake akiwa ameshikilia kisu mkononi mwake na kuwaita madaktari ambao walifika eneo la tukio na kumkimbiza hospitalini.
Hata hivyo, madaktari walishindwa kumuokoa mchinjaji huyo huku polisi wakianzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo ili kubaini chanzo cha kifo cha mchinjaji huyo.
Wizara ya Kazi ya Hong Kong ilitoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na kudokeza kuwa imeanzisha uchunguzi wake kuhusu tukio hilo.
"Tutafanya uchunguzi haraka iwezekanavyo ili kubaini chanzo cha mkasa huo, kubaini waliohusika na kupendekeza hatua za kuboresha ulinzi wa wafanyikazi," mamlaka ilisema kwenye taarifa. Kwa sasa haijulikani iwapo nguruwe huyo alifanikiwa kutoroka kuchinjwa.
Social Plugin