Watu waliokuwa wamejihami na silaha walimchoma moto padri wa Kanisa Katoliki hadi kufa na kumpiga risasi na kumjeruhi mwenzake kaskazini-magharibi mwa Nigeria siku ya Jumapili, Januari 15.
Polisi walisema, tukio hilo limeibua wasiwasi kuhusu usalama huku taifa hilo likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu mwezi ujao.
Msemaji wa polisi wa jimbo la Niger, Wasiu Abiodun alisema kuwa watu waliokuwa na silaha waliteketeza makazi ya Padre Isaac Achi, wa Kanisa Katoliki la Watakatifu Petro na Paulo, katika eneo la serikali ya mtaa wa Paikoro, baada ya kushindwa kuingia mwendo wa saa tisa asubuhi.
Padre Achi alichomwa moto hadi kufa huku padri mwenzake aliyefahamika kwa jina la Padre Collins aliyekuwa kwenye nyumba hiyo akipigwa risasi na kujeruhiwa alipokuwa akijaribu kutoroka.
Adiodun alisema padre Collins anaendelea kupata nafuu hospitalini.
"Huu ni wakati wa kusikitisha. Kwa padri kuuawa kwa namna hii ina maana kwamba sisi sote hatuko salama. Magaidi hawa wameipoteza, na hatua kali zinahitajika ili kukomesha mauaji haya yanayoendelea," alisema gavana wa jimbo la Niger Sani Bello.
Sababu ya shambulio hilo la Jumapili haikufahamika lakini mara nyingi majambazi hao wamekuwa wakiwalenga viongozi wa dini la Kikristu katika eneo la kaskazini lenye Waislamu wengi.
Raia wa Nigeria wanatazamiwa kupiga kura kumchagua rais mpya mnamo Februari 25, 2023.
Hata hivyo taifa hilo la magharibi mwa Afrika linakumbwa na visa vya utekaji nyara kwa na mauaji yanayotekelezwa na magenge ya wahalifu wenye silaha kaskazini mwa nchi hiyo.
Hali hiyo imezua hofu kuwa huenda uchaguzi utakosa kufanyika katika baadhi ya maeneo.