Polisi nchini Zambia wamemkamata mwanamume mmoja baada ya kuteketeza nyumba ya shemeji yake alipoamriwa kuondoka.
Titone Kapanshya, 22, alikuwa amehamia katika nyumba ya marehemu kaka yake baada ya uamuzi wa familia wa kufanyia boma hilo tambiko la utakaso.
Kwa mujibu wa Mwebantu, baada ya kufanya tambiko hilo la kitamaduni, mjane huyo alimtaka kijana huyo kuondoka nyumbani kwake, lakini alikataa. Katika hali hiyo ya mvutano, Kapanshya alitishia kujiua au kuteketeza nyumba hiyo iwapo atalazimishwa kukaa mbali na shemeji yake.
Kulingana na polisi, Kapanshya alitaka kuendelea kuishi na shemeji yake. Afisa mkuu wa mkoa wa Luapula Gloria Mulele alisema kijana huyo alitekeleza tishio lake kwa kuchoma nyumba ya mjane huyo baada ya kurejea kutoka kwenye ulevi saa 10 usiku. Mkuu wa polisi alisema ilichukua juhudi za majirani kuzima moto huo na pia kuuzuia kuenea kwa nyumba zingine.
“Familia ilimchagua Bw Kapanshya kwenda kumsafisha mlalamishi mnamo Disemba 10, 2022, na wakaanza kuishi pamoja na mke wa marehemu kaka yake. Baada ya siku kadhaa aliambiwa aondoke nyumbani kwa sababu alikuwa amemsafisha lakini alikataa kwa vile alitaka kuendelea kuishi na mke wa marehemu kaka yake kama mke wake mwenyewe," Mulele alisema.
Alieleza zaidi kwamba mjane huyo alikataa kuishi naye zaidi kwani tayari alikuwa amemsafisha. "Alimtoa nje ya nyumba yake. Bw Kapanshya alikasirika na kumtishia kwamba angejiua au kuchoma nyumba," alisema.
Social Plugin