Polisi nchini Kenya wanachunguza kifo cha mwanamitindo kijana na mwanaharakati wa wapenzi wa jinsia moja (LGBTQ) Edwin Chiloba baada ya mwili wake kupatikana umetupwa kando ya barabara karibu na mji wa Eldoret.
Sababu ya mauaji hayo haijajulikana, msemaji wa polisi amenukuliwa na gazeti la Star akisema. Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya, ambapo mapenzi ya jinsia moja hayaruhusiwi, wanahusisha kifo chake na kujihusisha kwake na mapenzi ya jinsia moja.
Kundi moja linakadiria kuwa zaidi ya nusu ya Wakenya wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja wamevamiwa.
"Maneno hayawezi hata kueleza jinsi sisi kama jumuiya tunavyohisi kwa sasa. Nafsi nyingine iliyopotea kwa sababu ya chuki," shirika la kutetea haki la galck+ lilichapisha kwenye Twitter.
"Kifo cha Edwin kinatukumbusha kwamba jamii hii inaendelea kushambuliwa kote nchini," Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu inayosimamia watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja iliandika kwenye Instagram.
Heshima kwenye mitandao ya kijamii zinamwelezea Chiloba kama "mbunifu wa kipekee".
Mwezi uliopita kwenye Instagram Chiloba aliandika kwamba "atapigania watu wote waliotengwa" akisema kwamba yeye mwenyewe alikuwa ametengwa.
Mwili wake uligunduliwa siku ya Jumatano.
Chanzo - BBC SWAHILI