GGML: UWANJA MPYA WA GEITA GOLD FC KUKAMILIKA MEI, 2023


Na Mwandishi wetu - Geita

UWANJA wa Magogo unaojengwa na Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kushirikiana na Kampuni ya Geita Gold Mine Limited , unatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu.


Hayo yamebainishwa hivi karibuni mjini Geita na Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti anayeshughulikia Miradi Endelevu ya Ghana na Tanzania, Simon Shayo alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Geita Gold FC na Coastal Union ya Tanga ambapo matokeo yalikuwa 1-0.


Alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa uwanja huo unaojengwa katika eneo la Magogo, kata ya Bombambili, mjini Geita mkoani Geita, ipo mbioni kukamilika.

Alisema wanajenga uwanja bora na salama kwa watumiaji na kwamba kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi ikisimamiwa na mshauri ambaye ameajiriwa na halmashauri ili ashauri namna ya kumalizia awamu ya kwanza na awamu nyingine.


“Kwa kushirikiana na halmashauri na uongozi wa mkoa wa Geita, nia yetu kuhakikisha hadi kufikia Mei mwaka huu uwanja uwe umekamilika na kuanza kutumika. Kwa hiyo hii itategemea sana kasi ya wakandarasi wetu na wote tunaofanya nao kazi ambao tunaamini kwamba watahakikisha uwanja huu unakamilika kwa wakati kwani nia yetu ni kuwa na uwanja bora, hatutaki kufanya kwa kuikimbiza na kuwa na eneo ambalo watu wanaweza kupata majeraha au uwanja ambao unaweza kuwa na dosari siku zijazo. Kama mjuavyo sisi tunu yetu ya kwanza ni usalama, kwa hiyo tungependa kuona wachezaji na mashabiki wanafanya shughuli zao kwenye uwanja ambao ni salama",alisema.

Aidha, akizungumzia udhamini wa zaidi ya Sh milioni 800 ambao kampuni hiyo ya GGML imetoa kwa Klabu ya GGFC, Shayo amesema sasa anaona timu inafanya vizuri.


“Tumeona timu inafanya vizuri, tulishuhudia wachezaji walivyocheza mechi zilizotangulia, tumeambiwa wachezaji wanazidi kusomana na kadiri timu inavyokaa pamoja tunaamini kwamba itaendelea kuimarika zaidi. Nia yetu ni kuona kwamba Geita Gold FC inatwaa ubingwa wa Tanzania bara badala ya kuishia nne bora, licha ya kwamba mimi ni mshabiki wa Simba SC. Tunaamini siku za karibuni watu wakija Geita watakuwa wanacheza na bingwa wa ligi kuu Tanzania bara,” alisema.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi, akizungumzia ujenzi wa uwanja huo na faida zake alisema utazidi kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Geita.


Alisema fursa hizo zitatokana na kuja kwa wageni wengi kutokana na michuano ya Ligi Kuu itakayokuwa inaendelea kuchezwa katika uwanja huo.

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa uwanja huo inakadiriwa kuwa Sh bilioni 2.4 ambazo zimetolewa na GGML kwa asilimia 80 kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii, ikishirikiana na Halmashauri ya Mji wa Geita.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post