Na Woinde Shizza , ARUSHA
Nabii Mkuu wa Kanisa la Ngurumo ya Upako Dkt. Geordavie Kasambale ameiomba serikali kuanza kuchunguza na kuyafuatilia makanisa yanayouza visaidizi kama maji ,mafuta ,chumvi na vinginevyo kwani asilimia kubwa ya makanisa hayo ni ya matapeli na wanapotosha jamii pamoja na kutumia mgongo huo kukwepa Kodi ya serikali.
Aliyasema hayo leo katika Ibada ya Jumapili wakati akiongea na waumini wa kanisa hilo ambapo amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya makanisa ambayo viongozi wake wamekuwa wakitumia visaidizi kuwadanganya waumini mbaya zaidi wamekuwa wakitumia mgongo wa kanisa kufanya biashara mbalimbali huku wakitumia njia ya makanisa kutolipa Kodi ya Serikali.
Alibainisha kuwa ni vyema kanisa likabaki ni mahali pa kutoa na kufundisha neno la Mungu na sio sehemu ya kufanya biashara kama baadhi ya viongozi wa dini wanavyofanya biashara za kuwauzia waumini visaidizi kama mafuta ,chumvi ,juice sabuni na vinginevyo.
"Nipende kuwaambia tu baadhi ya viongozi wa dini kama nguvu ya Mungu ipo ndani yako itabaki nguvu za mungu na kanisa litaendelea ata ukifiatilia kwenye vitabu vyetu vya dini hakuna sehemu ambayo inasema Yesu aliuza mafuta ,maji Wala chumvi katika kipindi chake ,Wala hakuna Mahali Yesu aliwakusanya watu wakafa kisa kugombania mafuta ,niseme tu wanaofanya hivyo ni matapeli tu hivyo ni vyema watu wakaamka wakasimama kwenye msingi wa zamani ambao ni neno la Mungu ", alisema nabii Mkuu Dkt. Geordavie
Alibainisha kuwa wakati umefika kwa watanzania na waumini kuachana na visaidizi na waridhike na nguvu za Mungu wanayohubiriwa na wachungaji wao.
"Niwatake tu viongozi wa dini ambao wanauza visaidizi hivyo wawe wafanyabiashara wa kawaida kama wameamua kuwa wauza maji na walipe kodi ya serikali kama inavyotakiwa na wasitumie mgongo wa kanisa kukwepa kodi ya serikali ", alisema.
Alisema kuwa iwapo serikali itawaachia hawa viongozi wakaendelea kufanya vitu hivi ipo siku maafa makubwa yanaweza kutokea kwani hata maafa yaliyotokea katika baadhi ya nchi yaliyotokana viongozi wa dini kuwadanganya waumini wao.
Pia aliwataka viongozi wa dini mbalimbali kuwahudumia waumini wao kimwili na kiroho ambapo alifafanua kuwa kiroho ni kuwalisha neno la Mungu ,kimwili ni kuwasaidia waumini wao katika suala zima la mitaji ili kuweza kuwakwamua katika umaskini.