Mwanamke anayefahamika kwa jina la Scholastica Peter mwenye umri wa Miaka 28 mkazi wa mtaa wa Bugwandege kata ya Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga, amewajeruhi watoto wake wawili kwa kuwachoma moto kwenye mikono kwa kile alichodai alikuwa akiwaonya baada ya kukomba mboga.
Waandishi wa habari wamefika eneo la tukio na kuzungumza na Mama huyo ambaye amekiri kuwachoma
moto watoto hao, akisema alifanya hivyo kama hatua ya kuwaonya, kwa sababu wana
tabia ya udokozi wa mboga.
“Hawa watoto wana tabia ya udokozi ile siku nilipika mboga tukala usiku
tukaibakiza asubuhi nikatoka nikaenda kutembeza mboga nikakuta wameikomba mboga
yote ilikuwa ni mboga ya dagaa nilichanganya na nyanya ntole/chungu sasa nilikuwaga
nawakanya hawasikii hiyo siku nilishikwa na hasira mara ya kwanza niliwapiga
na ya pili hii mara ya tatu kulikuwepo jiko lilikuwa na moto na kulikuwepo na
jiko ambalo nilikuwaga natolea mkaa baada ya kuwapiga nikasogeza hilo jiko
ndiyo nikawa nawababua na kijiko”,amesema Scholastica.
Akizungumzia tukio hilo mtendaji wa kata ya Ibinzamata Victor Kajuna
amesema kuwa taarifa hizo amezipata leo kutoka kwa wananchi waliochukua jukumu
la kuwabeba watoto na kuwapeleka katika ofisi ya afisa mtendaji wa kata.
“Leo majira ya saa nne asubuhi niliwapokea wananchi kutoka mtaa wa
Bugwandege walifika wakiwa wameongozana na mama mmoja pamoja na watoto wake
wawili wakaeleza kuwa baada ya watoto hao kuwaona wanaendelea kuishi bila
msaada”,amesema.
Diwani wa kata ya Ibinzamata Mheshimiwa Ezekiel Sabo amekemea kutokea
kwa tukio hilo huku akiwaomba wananchi wa kata hiyo kuacha tabia ya kutoa
adhabu kali kwa watoto wao,kwani kwa kufanya hivyo ni ukatili.
“Taarifa hii ya watoto kuchomwa moto nimeipokea kwa masikitiko makubwa
sana lakini nakemea swala hili lisijitokeze tena katika kata ya Ibinzamata kwa
sababu jamii ikifikia hapo basi tutakuwa tumefika pabaya sana na niviombe
vyombo vya serikali vifuatilie ili ukatili huu usijirudie tena”, amesema Sabo.
Kwa upande wake Afisa elimu wa kata ya Ibinzamata Mackrine Shija amewaomba
wazazi na walezi kuacha tabia ya kutoa adhabu kubwa kwa watoto.
Msaidizi wa kisheria kutoka Community Edification Organization kata ya
Ibinzamata Robert Said amesema kitendo hicho ni ukatili wa kijinsia.