Jeneza la mfalme wa soka duniani hayati Pele.
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva Jumanne anaongoza mazishi ya bingwa wa kandanda Pele ambaye atakumbukwa kama mchezaji bora zaidi katika historia ya kandanda.
Baada ya siku tatu za maombolezo, wananchi wa Brazil walitoa heshima zao za mwisho kwa Pele ambaye amepewa jina la mfalme, aliaga dunia Alhamisi wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 82, baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu.
Sherehe za Jumapili za kuapishwa Lula kuchukua madaraka zilianza kwa dakika moja ya kukaa kimya ili kutoa heshima kwa Pele, na leo yuko mji wa kusini mashariki wa Santos, ili kutoa heshima zake za mwisho kwa mfalme huyo wa kandanda kabla ya muda wa maombolezo uliowekwa ambao ulimalizika rasmi saa tatu asubuhi kwa saa za Brazil.
Maelfu ya waombolezaji pamoja na maafisa wa ngazi ya juu kwenye fani ya kandanda akiwemo rais wa FIFA Gianni Infantino wamepita karibu na jeneza la Pele ili kutoa heshima zao za mwisho kwenye uwanja wa michezo ya Vila Belniro ambako Pele na timu yake ya Santos FC waliutumia kwa muda mrefu.Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva akitoa hotuba baada ya kuapishwa wakati wa sherehe za uzinduzi wa urais wake katika Bunge la Taifa mjini Brasilia, Jan. 1, 2023.
Akizungumza na wanahabari alipofika kutoa heshima zake, Infantino alisema kwamba Pele atakumbukwa milele, akiongeza kwamba FIFA itaomba mataifa wanachama yakipatie angalau kiwanja kimoja cha mpira nchini humo jina la Pele kama njia ya kumkumbuka.
Gianni Infatino, kiongozi wa FIFA alisema: “Nafikiri ameacha wasia wa kipekee wakati akifanya mambo ambayo asilimia 99 ya wachezaji hawawezi kuyafikia kamwe. Asilimia 1 ya wachezaji wanaweza kufanya tu labda jambo moja alilofanya. Pele alikuwa wa kwanza kufanya aliyoyafanya na kwa hakika atabaki moyoni mwetu.
Tutahakikisha kwamba jina lake litabaki milele kwenye ulimwengu wa soka. Hiyo ndiyo sababu kubwa kwetu sisi kuwa hapa. Tunatoa heshima zetu kwa kuyaomba mashirika yote ya soka kuwa na dakika moja ya ukimya.”
Kundi kubwa la wachezaji, wanasiasa, watu mashuhuri pamoja na mashabiki wa kandanda wamesafiri hadi mji wa Santos na kusubiri kwa saa nyingi ili kumuaga Pele japo baadhi wameathiriwa na sherehe za kuukaribisha mwaka mpya.
Nahuel Nunes mwenye umri miaka 35 kutoka Argentina ni mmoja wao. Nunes ambaye ni shabiki wa soka anaeleza:
Namheshimu sana kama mshindi wa kombe la dunia mara tatu. Timu yetu ya Argentina pia ni washindi wa kombe hilo mara tatu. Japo sisi tumeshinda kwenye kombe la dunia lililomalizika hivi karibuni, bado ni na heshima kubwa sana kwake. Ilinibidi kufika hapa ili kuhudhuria tukio hili la kihistoria.
Jeneza la Pele lilipelekwa kwenye uwanja huo Jumatatu likiwa limebebwa na watu waliovalia mavazi meusi wakiongozwa na mwanawe wa kiume Edinho.
Mke wake Marecia Cibele Aoki ambaye ni wa tatu na aliolewa 2016 alionekana akisononeka wakati akikaribia kuushika mwili wake pale jeneza lilipofunguliwa.
Jeneza hilo lililofunikwa kwa bendera za Brazil pamoja na ile ya Santos pia lilizungukwa na mashada ya maua yenye rangi tofauti kutoka kwa watu mashuhuri kama mchezaji wa PSG ya Ufaransa na pia nyota wa sasa wa Brazil Neymar, ambaye alikuwa ameandamana na baba yake.
Mazishi yalianza asubuhi kwa saa za huko huku baadhi ya waombolezaji wakiwasili kwenye uwanja huo tangu Jumatatu ili kutoa heshima zao za mwisho kwa Pele, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Edson Arantes do Nascimento.
Msafara wa jeneza lake litazunguka mji wa Santos na utapitia karibu na nyumba ya mama yake Celeste Arantes mwenye umri wa miaka 100 na ambaye yupo hai licha ya kwamba haelewi kwamba Pele amefariki.
Mazishi yatafanyika kwa mujibu wa madhehebu ya Kanisa Katoliki kwenye makaburi ya Santos ambako mwili wa Pele utahifadhiwa kwenye Jumba maalum.