WAHUNI WASHIRIKIANA NA WANAFUNZI KUVUTA BANGI SHINYANGA MJINI

Mfano mwanafunzi akivuta bangi
Mwenyekiti wa mtaa wa Dome Solomon Najulwa akizungumza kwenye kikao cha mtaa huo

Na Suzy Luhende, Shinyanga Press Club Blog

Mwenyekiti wa mtaa wa Dome kata Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Solomon Najulwa amewataka wanafunzi wote wa mtaa wa Dome waliofaulu kuingia kidato cha kwanza kujiepusha na uvutaji wa bangi na madawa mengine ya kulevya kwa sababu yanavuruga ufahamu wa akili.

Hayo ameyasema Januari 5,2023 kwenye kikao cha kuwajengea uwezo wazazi na watoto wanaoingia kidato cha kwanza na wanaoanza chekechea kilichofanyia ofisini kwake kikiwahusisha wazazi wenye watoto hao, ambapo amewataka watoto kujiepusha na uvutaji wa bangi na utumiaji wa madawa mengine ya kulevya.

Najulwa amesema kuna vijana wengi wamemaliza darasa la saba wamejiingiza kwenye makundi mabaya ya uvutaji bangi, hivyo si vyema kujiingiza kwenye makundi hayo kwani yanaharibu tabia njema.

"Nawaombeni sana watoto wangu msijichanganye na makundi mabaya ya uvutaji bangi na madawa ya kulevya kwani yanaathiri nguvu kazi ya Taifa letu, mnatakiwa kusoma kwa bidii ili kwa baadae tujenge Taifa lenye umoja na lenye uelewa na nyinyi ndiyo mtakuwa sadaka nzuri kwa Taifa na kupata viongozi wazuri kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu,"amesema Najulwa.

"Pia nawaomba wazazi msiwaruhusu kulala kwa muda wanaotaka wao wenyewe lazima wapate muda mzuri wa kujisomea masomo ya kujikumbusha, aidha wazazi tusiwatume kupita kiasi watoto wetu na kukosa muda wa kujisomea,"amesema Najulwa.

"Baadhi ya watoto wetu wamekuwa wakijifungia ndani na simu kubwa wanajifunza mambo yasiyofaa na wanachati yasiyowafaa na wanaangalia mambo mabaya yasiyowahusu hayo yanapeperusha elimu yenu acheni kabisa, pia wazazi naomba muwe na ushirikiano na walimu toeni mchango wa chakula ili watoto waweze kupikiwa chakula kizuri na waweze kuwasilikiza walimu wanachokifundisha," ameongeza.

Mwalimu mkuu wa shule ya Bugoyi A Alex Juma amesema vijana wengi waliomaliza darasa la saba wanavuta bangi na wanavuta sana hadi wanaanguka na wanarudi shuleni hapo kuvutia, hivyo wazazi wanatakiwa kukaa karibu na watoto hao ili kuweza kuwabadilisha.


"Ni jambo la kusikitisha sana pale tunapoona mtoto mdogo namna hii akivuta bangi na hawaogopi hata mchana kweupe wanakuja hapo Bugoyi na wengine wamemaliza shule ya msingi mwaka jana tu nawaomba wazazi tuwasaidie watoto hawa hata wanapotoka nyumbani tuwafuatilie wameelekea wapi,"amesema Mwalimu Juma.


Mwalimu mkuu wa shule ya Bugoyi B Elisiana Mlangeni amesema watoto hao wamekuwa ni shida  katika eneo la Bugoyi, kwani wanakaa pale karibu na jiko wanaanza kuvuta bangi. "Siku moja walifukuzana na polisi lakini wanaendelea kuja tu imekuwa ni kero kubwa sana".


" Najiuliza hili ni kosa la wazazi au la mwanafunzi, naomba wazazi mfuatilie watoto hawa kwani tunajenga kizazi kibaya hawa watoto wakiendelea hivyo watakuja kuvunja maduka ya watu watakuwa wezi, wasaidieni mapema zungumzeni nao walekezeni watabadilika,"amesema Mlangeni.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa kikao hicho mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mazinge James Msimba ambaye alikuja kwa niaba ya mratibu elimu kata amesema ugumu wa maisha kwa wazazi sio kipimo cha kushindwa kulea watoto, kwani watoto wengi wamejikuta wakiwa katika mazingira mabaya kwa sababu wazazi wamewaacha na kuwa busy na maisha.

"Watoto hawa wanaosemekana wanavuta bangi wengi wao wanakuja shuleni kwangu Mazinge, hivyo wakileta mambo ya bangi shuleni kwangu nawafukuza, hivyo kabla hawajaja wazazi kaeni nao wakija huko waje wamebadilika wakiwa na maadili mema waje wapate haki yao ya elimu,"amesema mwalimu.

Baadhi ya wazazi Joseph Malale na Rea Enosi wamesema wanashukuru kukumbushwa, hivyo wameahidi kufuatilia watoto wao na kuwaelekeza, pia wameahidi kushirikiana na walimu ili kujua maendeleo ya watoto wao shuleni, lakini pia wamewaomba walimu pale watoto wao wanapoonekana wanakosea shuleni waonywe ili wasiendelee kufanya makosa.

Naye kamanda wa jeshi lapolisi mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi ameahidi kulifuatilia suala la watoto wanaovuta bangi wiki ijayo ataanza msako ili kuhakikisha anawakamata watoto hao na wale wanaosababisha kuvuta bangi watakamatwa.
Wakazi wa mtaa wa Dome wakimsikiliza mwenyekiti akizungumza na kuwaasa wanafunzi waache kuvuta bangi
Wazazi na wanafunzi wakimsikiliza mwenyekiti wa mtaa wa Dome akiwataka washirikiane na walimu

mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mazinge James Msimba akizungumza kwenye kikao cha mtaa wa Dome cha kuwajengea uwezo wazazi na wanafunzi waliofaulu kuingia kidato cha kwanza
Mwalimu mkuu wa shule ya Bugoyi (A) Alex Juma akizugumza kwenye kikao cha mtaa wa Dome
Mwalimu mkuu wa shule ya Bugoyi B Elisiana Mlangeni akiwaasa wanafunzi kutojiingiza kwenye makundi yasiyofaa

Wanafunzi wakiapa watasoma kwa bidii hawatajiingiza kwenye makundi yasiyofaa

Wanafunzi wakiapa watasoma kwa bidii hawatajiingiza kwenye makundi yasiyofaa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post