Profesa Christopher Kasanga, akiwa na mke wake aliyemuoa kwa siri
Mahakama ya wilaya ya Morogoro imempandisha kizimbani Profesa Christopher Kasanga wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa shtaka la ugoni baada ya kufunga ndoa ya pili kwa siri na mwanamke mwingine Oktoba 29 mwaka 2022.
Imeelezwa kuwa kesi hiyo ya madai namba 57/2022 imefunguliwa Desemba 16, 2022 na Matlida Sigareti dhidi ya mumewe Profesa Christopher Kasanga ambaye wamefunga ndoa miaka 25 iliyopita.
Bi. Matlida amelazimika kufungua keshi hiyo baada ya kubaini mume wake Profesa Kasanga kufunga ndoa nyingine kwa siri na mwanamke mwingine anayefahamika kwa jina la Linael Makundi ambaye ni mfanyakazi wa Benki ya CRDB.Mjini Morogoro.
Kesi hiyo inasikilizwa chini ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Morogoro Emmael Lukumai, ambapo katika upande wa mashtaka kesi hiyo inasimamiwa na wakili Emmanuel Chengula na Gervas Semgabo wakati upande wa utetezi ikisimamiwa na wakili Asifiwe Alinanuswe.
Akizungumza nje ya mahakama hiyo Wakili wa mlalamikaji Emmanuel Chengula amesema kesi hiyo imesikilizwa kwa mara ya kwanza mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo ambapo mteja wake ambaye ni Matlida Sigareti anadai kulipwa fidia ya shilingi milioni 100 za Kitanzania kutokana na madhara ambayo ameyapata.
Kwa upande wake Wakili wa utetezi Asifiwe Alinanuswe alipotakiwa kuzungumzia shtaka hilo alisema hajapewa maelekezo ya kuzungumzia kesi hiyo kutoka kwa mteja wake.
Hata hivyo, Hakimu Mfawidhi Lukumai ameahirisha kesi hiyo baada ya upande wa utetetezi kuweka pingamizi la kutaka kesi hiyo isikilizwe faragha ambapo imepangwa kusikilizwa tena Februari 21 mwaka huu.
Chanzo - EATV
Social Plugin