Wafanyabiashara wa soko la Samunge wakifurahia Hundi ya shilingi milioni mia iliyotolewa na Nabii Mkuu wa kanisa la Ngurumo ya upako ambaye pia ni balozi wa amani Dkt. GeorDavie
Balozi wa nabii Mkuu Sekela Ntondolo akionesha stakabadhi ya malipo ya kibenki (CRDB) ya shilingi milioni 100 iliyotolewa na Nabii Mkuu Kwa ajili ya wafanyabiashara wa soko la Samunge
Na Woinde Shizza ARUSHA
Nabii Mkuu wa Kanisa la Ngurumo ya Upako ambaye pia ni balozi wa amani Dkt GeorDavie Kasambale amekabidhi rasmi stakabadhi ya malipo ya kibenki (CRDB) ya shilingi milioni 100 aliyoiahidi kwa wafanyabiashara wa soko la Samunge jijini Arusha ambao walipata janga la kuunguliwa bidhaa zao na kupoteza mitaji yao mnamo mwaka 2019 .
Mbali na fedha hizo kugawiwa kwa wafanyabiashara pia kiasi cha shilingi milioni 20 kitatumika kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya soko ilo ikiwemo mageti na mitaro.
Akiongea wakati akikabidhi stakabadhi hiyo ya malipo kibenki kwa mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko la Samunge kwa niaba ya Nabii mkuu Dkt GeorDavie ,balozi wa nabii Mkuu Sekela Ntondolo aliwataka wafanyabiashara hao kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kujikwamua kiuchumi.
Aidha aliwataka wafanyabiashara hao wakafanye kazi kwa malengo yaliyokusudiwa pia wakafanye kazi kwa nguvu zao zote na wasimuingize shetani kwenye pesa hiyo ambayo nabii mkuu ameitoa kwani Mungu ndiyo amempa mtu wake ili aweze kuwasaidia katika biashara zao.
"Pia niwasihi tu wafanyabiashara ili mfanikiwe katika biashara zenu ni lazima mjitamkie mema ukifungua biashara yako jitamkie maneno mazuri ili ufanikiwe sema nitauza ,nitapata wateja ,nitafanikiwa lakini ukija ukijitamkia mambo mabaya na yatakukuta hivyo kila mmoja ajitamkie baraka mwenyewe ili afanikiwe na ulifanikiwa kupitia fedha hii msiache kusema ili Mungu awazidishie na pale mnapotoa ushuhuda kuwa ile pesa ya nabii mkuu imenitoa hatua moja kwenda nyingine itampa hata baba moyo wa kuwaongezea msaada na wengine",alisema Balozi Sekela.
Akiongea mara baada ya kukabidhi stakabadhi hiyo ya malipo mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo Njola Miraji, alimshukuru nabii mkuu kwa kutimiza ahadi yake ambapo alisema kuwa fedha hiyo inatarajiwa kugawiwa Kwa wafanyabiashara 1261 wa soko hilo ambapo alifafanua kuwa kati yao wafanyabiashara wa vyombo ni 95 ,mama lishe 86,vyakula vikavu 56, viongozi 23,wafanyabiashara wa viatu 85 ,wafanyabiashara wa nguo 397 pamoja wa mboga 519.
"Nimshukuru tu nabii Mkuu kwa kweli hatuna cha kumpa zaidi ya kumshukuru tangu tuunguliwe hakuna mtu yeyote amewahi kuja kutushika mkono pamoja hapa kuwa mkoani kwetu tumebahatika kuwa na mabilionea wa madini watatu wakiwemo wa Tanzanite na Rubby lakini wameshindwa kusaidia jamii yenye uhitaji ila uyu nabii Mkuu kweli katumwa na Mungu kaamua kuja kutusaidia sisi wananchi ambao tunahitaji na shida kweli Mungu aendelee kumbariki sana",alisema Njola.
Alibainisha kuwa katika fedha hizo wameorodhesha majina ya wafanyabiashara 1261watakaonufaika na fedha hizo na tayari majina yao ameyakabidhi kwa balozi wa kwa nabii mkuu ili amfikishie nabii Mkuu kama alivyoelekeza wakati akiahidi fedha hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa soko hilo Restuta Nyoni aliwataka wafanyabiashara hao ambao watapata fedha hizo kuziingiza katika mitaji yao huku akiwasisitiza kutotumia fedha hizo kufanya anasa.
Wakiongea kwa nyakati tofauti wafanyabiashara hao walimshukuru nabii Mkuu GeorDavie kwa moyo wake wa huruma na ukarimu na kuwataka wafanyabiashara na watumishi wengine wa Mungu kuiga mfano huo ili kuisaidia jamii yenye uhitaji.
Nabii Mkuu wa kanisa la Ngurumo ya upako ambaye pia ni balozi wa amani Dkt.GeorDavie alitoa ahadi hiyo Januari 23 mwaka huu katika soko hilo, baada ya kupokea maombi kutoka kwa wafanyabiashara hao juu ya uhitaji wa mitaji iliyopotea kutokana na kuunguliwa kwa soko hilo mwaka 2019 na kupoteza mali zao .
Social Plugin