Balozi wa Pamba nchini Tanzania Agrey Mwanri akizungumza kwenye kikao.
Balozi wa Pamba nchini Tanzania Agrey Mwanri akizungumza kwenye kikao.
Na Sumai Salum, KISHAPU
Balozi wa Pamba nchini Tanzania msimu wa mwaka 2022-2023 Agrey Mwanri amewataka viongozi kusimamia wakulima wa zao la pamba kulima kwa kufuata sheria katika maeneo yao ili kuepuka kulima zao hilo kiholela.
Mwanri amesema hayo leo Januari 9, 2023 katika kikao kazi maalum cha kujengeana uwezo kilichowakutanisha watendaji wa vijiji,wenyeviti wa vijiji,maafsa ugani pamoja na baadhi ya watumishi wa serikali ngazi ya halmashauri na wilaya katika ukumbi wa SHIRECU wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
“Wakati mwingine kutowajibika kwenu vizuri kunapelekea wakulima kulima kiholela, zao la pamba lipo kwa mujibu wa sheria za nchi na sio kienyeji sheria No.2 ya mwaka 2001 na ile ya 2011 zilitungwa kanuni 10 moja wapo ya kanuni inamtaka kila mkulima kung’oa na kuchoma maotea yote ya msimu uliopita ili kuua wadudu waharibifu kuhamia kwenye msimu mpya,kupanda kwa mstari pamoja na kupulizia dawa ya kuua wadudu”,amesema Mwanri.
Ameongeza kuwa wilaya ya Kishapu na Maswa kata ya Itilima bado kuna uelewa mdogo juu ya kulima kilimo chenye tija jambo lililopelekea waanzishe kuwepo mkulima mwezeshaji ambaye atakuwa ni chambo kwa wakulima wengine,kutoa elimu ya kutosha huku akiwaasha viongozi wawe mfano katika zao hilo kwa kwa kufanya hivo kutainua na kuongeza pato la mtu mmoja na taifa ikilinganishwa na mwaka 2021-2022.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya ugawaji na usambazaji viuadudu na vinyunyizi Bw Joseph Bukalasa alisema kamati hiyo yenye watu 10 kutoka taasisi mbalimbali za serikali imeundwa kwa maelekezo ya waziri wa kilimo Mhe. Hussein Bashe yenye lengo la kudhibiti na kuzuia uchepushaji wa upotevu pamoja na udhibiti ubora baada ya kupokea kutoka kwa mdhabuni kwenda kwa mkulima.
Aidha Katibu tawala wa wilaya ya Kishapu Bw Shadrack Kengese alisema kuwa ukosefu wa uadilifu katika kazi unapelekea uzembe ndani ya baadhi ya vyama vya msingi na kusababisha washindwe kufikia malengo yaliyokusudiwa katika zao hilo la pamba.
“Kwa bahati mbaya mikataba haioneshi kama kiongozi wa AMCOS akikosea atawajibika vipi mdhamini wake japo tutafika tuendako, maafisa ugani tusimamie kanuni za kilimo kwenye maeneo yetu iwapo wakulima kila siku wanamwaga mbegu na wewe uko pale je unastahili kuwepo pale? Kila mtu akisimamia kazi yake vizuri tutakuwa tumemsaidia Mhe. Rais kufikia malengo yale ambayo ameksudia katika sekta ya kilimo. ndugu zangu yamkini nimesema kwa ukali lengo hapa ni kumtaka kila kiongozi kutimiza wajibu wake”,amesema Mwanri.
Afisa Uchunguzi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutokea jijini Mwanza Bw Protas Henry ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya usambazaji pembejeo alisema kuwa lengo la serikali ni kuinua zao la pamba na wataalamu wamethibitisha kwa mkulima atakayefanya vizuri na kuzingatia kanuni mavuno yataongezeka.
“Lengo la serikali msimu wa 2022-2023 ni kuzalisha tani 500,000 kutoka tani 17300 Kishapu inatakiwa kuzalisha jumla ya tani 50,000 na hili tutafanikiwa baada ya wakulima kulima mapema, kupalilia na viuadudu na vinyunyizi kufika kwa wakati kwa walengwa na sisi kama kamati tutasimamia vema kugawa na kusimamia mtiririko wa ugawaji kwanzia ngazi ya wilaya,amkosi hadi kwa mkulima ili uzalishaji uweze kuongezeka, kwa yeyote atakaeenda kinyume na sheria hatutasita kumchukulia hatua stahiki”,amesema.
Hata hivyo wilaya ya Kishapu msimu wa kilimo 2021/2022 haikufikia malengo ya kulima hekari 100,000 kutokana na upungufu wa mvua,upungufu wa vinyunyizi kwa wakulima hivyo kutokana na kampeini ya balozi wa pamba ya octoba 2022 wakulima wameendelea kupewa elimu ya kutosha kukabiliana na changamoto hizo huku wakikusudia ongezeko kubwa la wakulima wa pamba kwa msimu wa 2022/2023.
Katibu tawala wa wilaya ya Kishapu Bw Shadrack Kengese akizungumza kwenye kikao hicho
Social Plugin