WASAMBAZAJI WA PEMBEJEO MANYARA WATAKIWA KUTOA ELIMU YA KILIMO BORA CHA BIASHARA


Afisa kilimo wa mkoa wa Manyara Paulina Joseph

Na John Walter-Manyara


Afisa kilimo wa mkoa wa Manyara Paulina Joseph amewaasa wauzaji na wasambazaji wa pembejeo kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo kutoa elimu juu ya kilimo bora cha biashara ikiwemo matumizi mazuri ya mbolea pamoja na viuatilifu kulingana na mazingira halisi ya eneo la mkulima husika.



Ameyasema hayo katika kikao maalum cha kutoa elimu kwa wauzaji wa pembejeo juu ya namna ya kutumia vizuri mfumo wa ulipaji wa mbolea ya ruzuku ili kuwasaidia wakulima wapate mbolea kwa urahisi kilichoandaliwa na maafisa kutoka katika kiwanda cha mbolea Dodoma kiwanda ambacho kinatazamiwa kuanza kusambaza mbolea hivi karibuni.



Aidha Paulina ametoa wito juu ya kufuatilia kwa usahihi taarifa za utabiri wa hali ya hewa ili ziwasaidie kuwaelimisha wakulima kujua ni wakati gani sahihi wa kupanda mazao kulingana na utabiri wa hali ya hewa kwa msimu husika kwani licha ya wao kuwa wafanyabiashara lakini pia ni wadau muhimu kwa serikali katika kutoa elimu.



Kwa upande wa wauzaji wa pembejeo za kilimo wamesema wapo tayari kwa sasa kufuata maagizo ya serikali haswa katika upande wa mbolea ili kuleta unafuu kwa mkulima lakini maboresho zaidi ya mfumo yanahitajika ili kuwezesha zoezi hilo lifanyike kwa urahisi bila kuonea upande wowote.


Kiwanda cha mbolea cha Dodoma ITRA kinakamilisha jumla ya viwanda viwili vya mbolea hapa nchini Tanzania vinavyotazamiwa kutoa kiasi kikubwa cha mbolea kitakachokidhi haja ya wakulima hapa nchini hivyo elimu iliyotolewa leo itarahisisha utaratibu mzuri wa usambazaji wa mbolea pindi itakapoanza kusambazwa rasmi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post