Na Dotto Kwilasa, DODOMA
WAZIRI wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki Dkt. Stergomena Tax amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi zote nchini pamoja na Taasisi za kimaendeleo kuhusu hali ya amani nchini na kueleza kuwa Tanzania bado ni sehemu ya amani duniani.
Hatua hiyo ni kufuatia kuwepo kwa taarifa za matishio ya kiusalama zinazoripotiwa kwenye vyombo vya habari na kupelekea shirika moja la ndege duniani kusitisha safari zake nchini.
Akiongea na Waandishi wa habari leo Jijini hapa mara baada ya kikao hicho, Waziri huyo amekanusha taarifa hizo na kueleza kuwa Tanzania ni salama na hakuna machafuko yoyote na kwamba shughuli zote za uchumi zinaendelea kama kawaida.
" Tumekutana na wadau wa maendeleo na kuwahakikishia kuwa nchi yetu ni salama,nasisitiza nchi yetu ni salama hakuna machafuko na kazi zote zinaendelea kama kawaida,watanzania puuzeni habari za mitandaoni ambazo hazina uthibitisho wa Serikali,"amesema.
Sambamba na hayo ametumia nafasi hiyo kuwataka watanzania na wadau wengine wa maendeleo kupuuza taarifa zisizo rasmi na kueleza kuwa ,"Tanzania kama nchi tunazo taratibu za kutoa taarifa hivyo ni marufuku kutoa taarifa zinazoweza kuleta taharuki, taarifa zote lazima dhithibitike na Serikali na si vinginevyo,"amesema
Pamoja na hayo amesema Serikali inathamini mchango wa wadau wa maendeleo kwamba ipo tayari kufanya nao kazi kwa ushirikiano hasa kwenye eneo la amani na usalama wao hivyo kuwataka kushirikiana na Serikali kama wanaona viashiria vya uvunjifu wa amani Kwa kutumia njia za kidiplomasia na si vinginevyo.
"Tumekubaliana kwamba tufanye kazi kwa pamoja na kuepusha taharuki,niwahakikishie watanzania wote na Dunia nzima kwamba Tanzania ni salama na hakuna matishio yoyote na tumeendelea kupokea wageni wengi,"amesema Waziri huyo.
Social Plugin