Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog Kishapu
Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga leo January 12,2023 imeadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar kwa kupanda miti pembezoni mwa eneo la Bwawa la maji kijiji cha Kishapu, ambapo zaidi ya miche 1000 ya miti imepandwa.
Katika zoezi hilo liliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Modest Mkude ameambatana na Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwepo katibu Tawala wa Wilaya, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkurugenzi Mtendaji, Wakuu wa Idara na Taasisi mbalimbali Wilayani Kishapu.
Akizungumza baada ya zoezi la upandaji miti amewashukuru wote kwa waliojitokeza katika zoezi hilo.
"Ninawashukuru sana Ndugu zangu wote mliojitokeza katika zoezi hili la upandaji wa miti lakini nitoe wito Wananchi wote kuzitumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kupanda miti hasusani miti ya matunda lakini pia miti hii inayotunza maji tuendelee kupanda katika Vyanzo vyote vya maji", amesema Mkude.
Amesisitiza kuwa jitihada kubwa za Serikali ambazo zinafanywa kulinda mazingira ziungwe mkono na wananchi kwani ni jukumu la kila mmoja.
Aidha Mkuu wa Wilaya amewataka Wananchi wote wanaozamia katika eneo hilo kwaajili ya kufanya kilimo na makazi kupisha mara moja kuepusha uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, amesema kuwa kwa ujumla maeneo ya Wilaya ya Kishapu yana mvua kidogo, katika kilimo wanategemea sana kilimo cha umwagiliaji.
"Kwa ujumla kama tunavyofahamu Wilaya ya Kishapu ni kame ina mvua kidogo kwa hiyo tunategemea sana kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia mabwawa na mkakati uliopo ni kuhakikisha kuna mabwawa ya kutosha kila sehemu na jitihada ambazo zinafanyika kwa sasa ni kufufua mabwawa yaliyoharibika, tumefufua Bwawa la Kiloleli, Mihama na Beledi", amesema.
"Kwa Mwaka huu Halmashauri imetenga Fedha kwa ajili ya kufufua mabwawa zaidi kauli mbiu yetu ni kuhakikisha Wilaya yetu inakuwa na mabwawa zaidi kwaajili ya kilimo na ufugaji", ameongeza.
Naye Diwani wa kata ya Kishapu Mheshimiwa Joel Charles Ndettoson ameeleza kuwa Bwawa hilo linahudumia zaidi ya kata Nane mpaka na Wilaya jirani ya Maswa wote wanatumia Bwawa hilo
"Bwawa hili linasaidia zaidi ya kata nane, Bwawa hili mbali na wanakijiji wanaotumia Kuna Shughuli za kimaendeleo zinazotumika eneo hili tumeona leo tupande miti zaidi ya 1000 pia tumeweka mikakati ya kusimamia Bwana hili ili liendelee kutusaidia", amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kishapu Bw Elikana Masanja amefurahishwa na ujio wa Mkuu wa Wilaya pamoja na msafara wake kwa uamzi wa kupanda miti katika eneo hilo.
"Nafurahia sana kwa ujio wa Mkuu wa Wilaya katika Bwawa hili na kuamua kupanda miti katika eneo hilo kwa Sababu itasaidia sana katika utunzaji wa Vyanzo vya maji na Bwawa hili litarejea katika thamani yake", amesema.
Social Plugin