Na John Walter-Babati
Watu wawili wakazi wa Kijiji Endagile kata ya Mamire wilaya ya Babati mkoani Manyara, John Lulu na Zebedayo Safari, wamehukumiwa kifungo Cha miaka 20 jela kwa kosa la kukutwa na meno mawili ya tembo.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Januari 30,2023 na Mheshimiwa Hakimu Victor Kimario katika mahakama ya wilaya ya Babati baada ya ushahidi ulitolewa na Mashahidi nane Mahakamani hapo kuthibitisha pasi na shaka.
Imeelezwa Mahakamani hapo kuwa Meno hayo yanayodaiwa kuwa ni sawa na idadi ya tembo mmoja aliyeuwawa ambaye thamani yake ni shilingi milioni 35.1, walikutwa nayo walipokamatwa na askari wa wanyamapori katika kijiji cha Bulkeri 23,10,2022 wakiwa kwenye pikipiki.
Upande wa waendesha mashtaka wa Jamhuri Rusticus Mahundi na Abood Komanya waliieleza Mahakama kwamba kwa kuwa watu hao walimuua Mnyama tembo ambaye ni kivutio kikubwa kwa watalii kuja nchini na Mheshimiwa Rais wa Dr. Samia Suhulu Hassan alifanya jitihada kuutangaza utalii kwa Filamu ya royal Tour na pamoja na kuwa hawana rekodi zozote za nyuma za watuhumiwa hao, aliiomba mahakama iwapatie adhabu Kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Katika utetezi wake Mshtakiwa wa kwanza John Lulu aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ana Watoto wawili wanaosoma Sekondari, dada yake mlemavu,mama yake mzee wote wanamtegemea.
Mshtakiwa wa pili Zebedayo Safari aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa kwenye familia yeye ndo tegemezi.