Wenyeji wa Kijiji cha Eshitimba, Kaunti ya Kakamega wametamaushwa na kifo cha ajuza wa miaka 89.
Floice Lisero, alikufa moto baada ya mjukuu wake wa kiume mwenye umri wa miaka 40, kuteketeza nyumba yake kufuatia mzozo kuhusu pesa.
Mshukiwa huyo tayari amekamatwa na polisi, na inadaiwa alimshambulia bibi yake baada ya kukataa kumpa pesa alizomuitisha.
Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Khwisero Samuel Kogo alithibitisha mkasa huo, akisema kwamba polisi walimuokoa mshukiwa huyo kutoka kwa wanakijiji waliojaribu kumpiga kitutu katika soko la Ebukambuli.
Kamanda huyo alisema kwamba mwanamume huyo atapimwa akili kubainisha iwapo yuko sawa au tahira, kabla ya kufunguliwa mashtaka dhidi yake.
“Ni lazima tumpeleke akapimwe akili ili kuthibitisha iwapo ako timamu au la kabla ya kumfungulia mashtaka yoyote,” Kogo alisema.
Social Plugin