Mjumbe wa Baraza Kuu kutoka UWT Taifa Helen Bugoye akizungumza kwenye maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi CCM.
Na Sumai Salum, KISHAPU
UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi CCM (UWT) Mkoa wa Shinyanga, umeadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi CCM, huku wakilaani kuendelea kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto ikiwamo ubakaji na ulawiti.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Januari 30, 2023 katika viwanja vya Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi CCM wilayani Kishapu.
Akizungumza mgeni Rasmi kwenye maadhimisho hayo, Mjumbe wa Baraza Kuu kutoka UWT Taifa Heleni Bugoye, amelaani matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo, huku akiwataka wazazi kujenga tabia ya kulinda usalama wa watoto wao ili wasifanyiwe vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Wazazi tujenge tabia ya kuwasikiliza watoto wetu, pamoja na kuwaogesha wale wenye umri mdogo ili kuwakagua kuona kama hua wanafanyiwa vitendo vya ubakaji, ukimshika sehemu za siri na kuona anarudi nyuma tambua kuna shida,”amesema Bugoye.
Naye Mwenyekiti wa UWT wilayani Kishapu Rahel Madundo amewataka wazazi wawapeleke shule watoto wao, ili wasome na kutimiza ndoto zao na kuja kuwa tegemeo la familia na taifa, na wasipofanya hivyo ni kuwafanyia ukatili, na Serikali haitasika kuwachukulia hatua.
Aidha, katika sherehe hizo za miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM, Umoja huo wa wanawake UWT, pia umeadhimisha kwa kupanda Miti katika Hospitali ya Jakaya Kikwete wilayani Kishapu, pamoja na kutoa zawadi kwa wagonjwa katika Hospitali hiyo zikiwamo sabuni za kufulia, biskuti na Juice.
Nao Baadhi ya Wagonjwa akiwamo Zaituni Rashid amewashukuru wanawake hao wa UWT kwa kuwapatia msaada zawadi hizo, huku wakipongeza huduma za matibabu ambazo wanapewa katika Hospitali hiyo.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Jakaya Kikwete wilayani Kishapu Dk. Mohamed Mkumbwa, amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha na kuboresha huduma za matibabu katika Hospitali hiyo.
Social Plugin