Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Wakala wa Vipimo Makao Makuu Dodoma ili kujiridhisha na kasi na utendaji kazi katika mradi huo.
Dkt. Hashil ameipongeza WMA kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu na pia ameupongeza uongozi kwa jinsi wanavyoendeleza ujenzi wa Ofisi za Mikoa kwa lengo la kuboresha mazingira mazuri ya utendaji kazi.
Amesema kuwa ujenzi wa Ofisi ni muhimu sana na ujenzi wake unatumia fedha za Serikali ambazo ni fedha za walipa Kodi hivyo tunatakiwa tuzisimamie sana na tuhakikishe kila kitu kinachopaswa kufanyika kinafanyika ndani ya muda wake.
Amempongeza Mkandarasi kwa spidi nzuri ya ujenzi na amesema ni matumaini yake ujenzi utawahi kukamilika kabla ya muda waliojiwekea. Kadharika amemtaka Mkandarasi kuhakikisha manunuzi ya vifaa yanafanyika mapema ili kuondoa vikwazo vya ujenzi kuchelewa.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Bi. Stella Kahwa amemshukuru Katibu Mkuu Dkt. Hashil Abdallah kwa kutembelea ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu na kuhaidi kufanyia kazi maelekezo aliyotoa ili mradi uweze kukamilika kwa wakati.
Pamoja na hayo, Bi. Stella ameeleza kuwa ujenzi huu ulianza July 2022 na mpaka sasa kazi imefanyika kwa asilimia 38 hivyo kwa Kasi hiyo anaamini ujenzi utakamilika mapema kabla ya muda ila kwa ubora wa hali ya juu.
Ameeleza kuwa Jengo hilo litakuwa na Ofisi ya Makao Makuu lakini pia zitakuwepo Ofisi za Mkoa wa Dodoma. Vilevile, kutakuwa na maabara ya kisasa pamoja na mitambo ya kupima Mita za Umeme pamoja na Dira za Maji.
Imeandaliwa na Sehemu ya Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma
Social Plugin