Idara ya elimu Mkoa wa Dodoma imefanya kikao kazi cha wadau wa elimu Mkoa kilichohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akiwa ndiye mgeni rasmi wa kikao hicho kililichofanyika katika ukumbi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) eneo la Mipango Jijini Dodoma.
Katika kikao hicho kilicholenga kujadili mpango kazi wa muelekeo wa namna ya kuanza mwaka mpya wa masomo 2023, kimejadili mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wa Elimu kwa Mkoa wa Dodoma na kupanga mikakati ya kufanya vizuri kwa mwaka huu mpya.
Mkuu wa Mkoa amebainisha mambo kadhaa ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameboresha kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya elimu.
“Rais amefanya mambo mengi kuboresha sekta ya elimu kama vile kuondoa ada kuanzia shule za awali mpaka kidato cha sita, ujenzi wa madarasa ya kutosha kupokea idadi kubwa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza ambapo kwa awamu ya kwanza ya fedha za Uviko – 19 mwaka 2021 Mkoa wa Dodoma ulipata fedha za kujenga madarasa 776 na kwa mwaka huu tumepatiwa fedha shilingi Bilioni 15.6 kujenga madarasa 339. Pia Rais ametoa ruzuku kwa shule kila mwezi shilingi Milioni 200” Amesema Mhe. Senyamule
Aidha, Mkuu wa Mkoa ametoa hamasa kwa walimu kufanya kazi kwa bidii kwani wao ndio wanaoweza kusaidia kuinua Mkoa katika kupata matokeo mazuri kwenye mitihani ya kitaifa“Nasisitiza walimu ni kundi linaloweza kujenga nchi au kuibomoa. Nitoe rai kwa maafisa na walimu wakuu kusimamia uandikishwaji wanafunzi wa shule za awali na darasa la kwanza. Mpaka sasa wanafunzi walioandikishwa kwa shule za awali wamefikia 57,617 ambapo lengo ni kuandikisha wanafunzi takribani elfu 70 na kwa darasa la kwanza wameandikishwa wanafunzi 74,230 sawa na 82.4% wakati lengo ni kuandikisha wanafunzi 90,122 hivyo uandikishaji haujafikia lengo. Niwatake Halmashauri zote kufuatilia uandikishwaji ili tuweze kufikia asilimia 100 kwani Watoto bado wapo wengi amabo hawajaandikishwa” Amesisitiza Mhe. Senyamule
Social Plugin