KATAMBI: SERIKALI INAENDELEA KUWAJENGEA VIJANA MAZINGIRA WEZESHI NCHINI

 
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na uongozi na wanafunzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini wakati wa hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wapya wa mwaka wa masomo 2022/2023, jijini Dodoma.

Sehemu ya wanafunzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini wakisikiliza maelezo ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi (hayupo pichani) wakati wa hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wapya wa mwaka wa masomo 2022/2023.


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akimkabidhi cheti cha pongezi Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hosen Mayaya ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake katika malezi ya wanafunzi wa chuo hicho.


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobasi Katambi akiwa ameshika kombe pamoja na Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hosen Mayaya (kulia) mara baada ya kukabidhiwa na vijana wa chuo hicho walioshiriki mashindano ya SHIMIVUTA.


Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hosen Mayaya akieleza jambo wakati wa hafla hiyo.


Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (MISO), Bi. Sayuni Mmari akizungumza wakati wa hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wapya wa mwaka wa masomo 2022/2023, Dodoma.

.....................................

Na: OWM – KVAU -DODOMA

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa kipaumbele na kuweka mikakati mbalimbali ya kuwajenga vijana mazingira wezeshi yatakayo wawezesha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa na kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi wakati wa hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wapya wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa mwaka wa masomo 2022/2023 katika ukumbi wa Mwl. Nyerere uliopo chuoni hapo jijini Dodoma.

Mheshimiwa Katambi amesema, dhamira ya Serikali ni kuwapatia vijana elimu bora na thabiti inayoendana na mazingira yao na kuhakikisha elimu hiyo inawasaidia katika kuhudumia taifa na kuwapatia maarifa yatakayo wawezesha kujiongoza.

“Vijana ndio nguvu kazi ya taifa na Serikali ina matarajio makubwa na kundi hilo kwa kuwa ndio watakaoleta mapinduzi ya ukuaji wa uchumi wa nchi,” amesema

“Endeleeni kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa letu ya kuhakikisha masuala ya vijana yanapewa kipaumbele,”

Ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kuweka mikakati endelevu yenye malengo ya kuwezesha vijana ikiwemo kuwapatia mikopo yenye riba nafuu ambayo hutolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, vilevile mikopo inayotolewa na halmashauri mbalimbali zilizopo nchini kupitia mapato ya ndani (4% kwa vijana, 4% wanawake na 2% Watu wenye Ulemavu) ambayo imewezesha vijana kuanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali inayowaingizia kipato.

Ameeleza kuwa jitihada nyingine zilizofanyika ni pamoja na kuwezesha vijana kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ambayo kupitia mafunzo tarajari (Internship) yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA) imewezesha wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kushiriki mafunzo ya uzoefu wa kazi na baadhi ya vijana wameajiriwa na makampuni mbalimbali. Pia, amesema kitengo hicho kimeweza kuwaunganisha vijana na fursa za ajira nje ya nchi ikiwemo wakati wa kombe la dunia.

Vile vile, ameeleza namna vijana nchini walivyoweza kunufaika na fursa mbalimbali za ajira kupitia miradi ya kimakakati inayoendelea kutekelezwa nchini.

Aidha, Naibu Waziri Katambi amewataka vijana hao kutambua wajibu walionao na kuwa na tabia njema ili waweze kufanikiwa sambamba na kutimiza malengo yao.

Naye, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hosen Mayaya, ameshukuru Serikali kwa kuendelea kuwezesha sekta ya elimu nchini ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kukomboa taifa.

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (MISO), Bi. Sayuni Mmari ameeleza kuwa wanafunzi wa chuo hicho wataendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post