Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KATIBU MKUU CCM ASHAURI UZALISHAJI SUKARI NCHINI UENDANE NA KUPUNGUZA BEI


Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV-Kilosa

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo ametoa mwito kwa wazalishaji wa sukari nchini kuhakikisha sukari inayozalishwa inakwenda kushusha gharama au bei kwa mlaji.

Akizungumza Januri 30 ,2023 baada ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha sukari Mkulazi kwa ajili ya kusikiliza changamoto , Chongolo ametumia nafasi hiyo kueleza kuzalisha sukari ya kutosheleza ndani ya nchi yetu ni jambo linalokuwa na tija sana.

“Mwito wangu kwenu hakikisheni sukari inayozalishwa inaenda kushusha gharama au bei ya sukari kwa mlaji hilo ndilo jambo la msingi .Sukari sio starehe wala sio hanasa bali ni bidhaa ya matumizi ya mwananchi wa kawaida yoyote yule , mnajua asilimia kubwa ya vyakula tunavyokula vinahitaji sukari viwe vya kiwandani au viwe vya nyumbani kwa hiyo mahitaji ya sukari ni makubwa.

“Na kwasababu viwanda vinavyozalisha viko hapa nchini ni lazima tuweke msukumo kuhakikisha tunaendelea kusaidia kuhangaika kushusha bei ya bidhaa hiyo kwenye soko, tukizalisha vya kutosha na tukazalisha kwa bei ndogo maana yake na bei itakuwa chini,”amesema Chongolo.

Aidha ameuomba uongozi wa kiwanda hicho kwamba watakapozalisha umeme wao kiwandani hapo maana yake uzalishaji utakuwa wa gharama nafuu na wakianza kuuza umeme wasichukue faida yoyote kuweka mfukoni bali faida hiyo waitumie tena kupunguza gharama ya uzalishaji wa sukari ili baadae ipatikane sukari ambayo itakuwa na bei nafuu kwa ajili ya ununuzi.

“Watanzania watafurahi wakiona sehemu ya shughuli zinazofanywa nchini zinarahisisha pia maisha yao.Kuhusu changamoto ya umeme tumechukua na tutakwenda kuhangaika nayo,”amesema Chongolo.

Awali wakati Chongolo anaanza kuzungumza amezungumzia changamoto ya umeem ambayo amepewa wakati anasomewa taarifa ya kiwanda hicho ambapo pamoja na mambo mengine wamekuwa kwenye mchakato wa kuzalisha umeme megawati 15 ili uweze kutumika kwenye kiwanda hicho.

“Nimefurahi kusikia jitihada ambazo mnazifanya katika kuhakikisha mnakuwa na umeme wenu na kilichonifurahisha mmekwenda mbali zaidi, mnachotaka ni TANESCO kukaa na ninyi mkubaliane.Mmetenga mpaka fedha kwa ajili ya kujenga laini ya kupeleka umeme mpaka Msamvu ili muingize kwenye kituo cha kupokelea pale na kupooza na kuingiza kwenye gridi ya taifa

“Huu ndio uzalendo na huko ndio kufanya mambo ili yalete tija kwa haraka, kama matokeo ni chanya na uzalishaji umeenza , uwezo wa kuzalisha hizo megawati 15 unawezakana halafu watu wa kufunga ule umeme wakiwa taratibu maana yake hawatendeki haki

“Niwahakikishie muda mfupi ujao utaona kila mmoja akiwajibika kwasababu ndio wajibu wetu, tutaenda kukaa kwenye vikao vyetu na huko tutaona taratibu za kufanya lakini hatutakubali tukiona mambo yakikwama kwasababu za mtu hatekelezi wajibu wake,”amesema Chongolo.

Katibu mkuu wa CCM Daniel Chongolo kwenye Ziara hiyo ameambatana na Katibu wa halmashauri kuu ya CCM Taifa itikadi na Uenezi Sophia Mjema pamoja na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni Issa Haji Gavu kwa ajili ya kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho pamoja na kuzungumza na Makundi mbalimbali.


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo akizungumza mbele ya Uongozi wa kiwanda cha Sukari Mkulazi,kilichopo Wilayani Kilosa mara baada ya kutembelea kiwanda hicho na kujionea ujenzi unavyoendelea na uwekezaji mkubwa uliofanywa kiwandani hapo,Chongolo ametumia nafasi hiyo kueleza kuzalisha sukari ya kutosheleza ndani ya nchi yetu ni jambo linalokuwa na tija sana na kwamba wazalishaji wa sukari nchini kuhakikisha sukari inayozalishwa inakwenda kushusha gharama au bei kwa mlaji.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com