Na.Mwandishi Wetu -MTWARA
Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mhandisi Nobert Kalembwe amesema kuwa usafirishaji wa makaa ya mawe kwenda nje ya nchi kupitia bandari hiyo umeongeza mapato kwenye bandari hiyo sambamba na kuongezeka kwa kampuni za usafirishaji wa makaa ya mawe kwenda nje ya nchi.
Mhandisi Kalembwe aliyasema hayo leo tarehe 24 Januari, 2023 mkoani Mtwara kwenye mahojiano maalum ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kipindi maalum chenye lengo la kuangalia mchango wa Sekta ya Madini katika kuwawezesha watanzania kiuchumi pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii katika mikoa ya Njombe, Ruvuma na Mtwara.
Akielezea hali ya usafirishaji wa makaa ya mawe kwenda nje ya nchi alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022-2023 walipangiwa kusafirisha tani 402,000 na kusisitiza kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 2022 hadi Januari 2023 wamefanikiwa kusafirisha tani 721,000 ikiwa ni ishara ya kuwa biashara ya makaa ya mawe katika mikoa ya Njombe na Ruvuma imeendelea kukua.
Alisema kuwa makaa ya mawe yanasafirishwa kupitia kampuni za Ruvuma Coal Limited na Jitegemee Holding Company Limited na kuongeza kuwa kampuni nyingine zipo mbioni kuanza usafirishaji wa makaa ya mawe na kutaja kuwa ni pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Gold Walk Limited, SEBDO, Aria Commodities International Limited, Marine Tech, Market-Insight na BECO.
Alisema kuwa makaa ya mawe yamekuwa yakisafirishwa katika nchi za India, Senegal, Ufaransa, Misri, Poland, Zanzibar, Ghana, Kenya, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Netherland.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wasafirishaji wa makaa ya mawe kupitia bandari ya Mtwara sambamba na kupongeza kazi nzuri inayofanya na Ofisi ya Madini Mtwara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania – Mtwara hasa kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara ya makaa ya mawe waliongeza kuwa wamejipanga kuendelea kutoa huduma kwa watumiaji wa makaa ya mawe wa ndani na nje ya nchi.
Msimamizi Mkuu wa kampuni ya Aria Commodities kwa upande wa Mtwara Seleman Kikwete alisema kuwa kampuni yake inapokea tani kati ya 300 hadi 600 za makaa ya mawe kwa siku kutoka Songea mkoani Ruvuma ambapo mpaka sasa ina tani 59,000 ambapo inatarajia kusafirisha nje ya nchi na kusisitiza kuwa kampuni ipo tayari kuuza makaa ya mawe kwa viwanda vya ndani ya nchi.
Naye Meneja wa Kampuni ya Ruvuma Coal Company Limited- Tawi la Mtwara, Said Ghaddaf alifafanua kuwa tangu kuanza kwa kampuni hiyo takribani miezi 15 iliyopita, imeshasafirisha tani 990,000 za makaa ya mawe nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, aliishukuru Serikali kwa upanuzi wa bandari ambapo imekuwa na manufaa kwa wasafirishaji wa makaa ya mawe kwani imeongeza uwezo wao wa kusafirisha makaa ya mawe mengi zaidi.
Social Plugin