Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Freeman Mbowe amesema yeye sio kiongozi ambaye anaweza kununuliwa kwa chochote kama ambavyo baadhi ya wanachama wa chama hicho walivyomtazama baada ya kuonekana akifanya vikao mara kwa mara na Rais Samia.
Mbowe ameyasema hayo leo Januari 21 jijini Mwanza kwenye mkutano wa kwanza wa hadhara baada ya takribani miaka saba kwa vyama vya kisiasa kuwekewa katazo la kufanya mikutano ya hadhara.
Mkutano huo umefanyika katika uwanja wa Furahisha Jijini humo
"Wakati nyinyi mnaona kulikua na ugumu upande wenu upande wa CCM kulikua na ugumu kuliko CHADEMA kwasababu wanajua, yaani nyinyi badala ya kunipongeza Mbowe mnakuja kusema mambo ya kiharamia kwamba Mbowe anakula asali, hivi mnajua Mbowe anapoteza bilioni ngapi kwa CHADEMA"
"Nilivumilia kwasababu nilisema nina mambo makubwa ya kuyatafuta kuliko kauli za propaganda, nilisimama kuanzia miaka 30 iliyopita kuitafuta haki na ustawi wa nchi yangu nitasimama hapo kwa gharama yoyote hakuna idadi ya fedha wala mali itakayofanya niwasaliti watanzania," amesema Freeman Mbowe
Hata hivyo Mbowe amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu vyama vya siasa nchini kufanya mikutano ya hadhara baada ya mazungumzo yao ya muda mrefu ya kumshawishi na baadae kukubaliana naye licha ya baadhi ya wanachama wa chama tawala kutokubaliana na hatua hiyo.
"Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni nasimama mbele ya watanzania kumshukuru Rais Samia kwa namna ambavyo alikuwa mvumilivu kwenye vikao mfululizo nilivyokaa nae kumshawishi atambue kwamba nchi inahitaji maridhiano, huyu Rais akakubali maridhiano"
"Watu walitamani maridhiano yasifanikiwe kwasababu kuna kitu wanafaidi lakini Rais Samia nimempelekea kwa niaba yenu wote alafu watu wanataka nimtukane siwezi kufanya hivyo" amesema Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe
Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA leo kinaadhimisha mika 30 tangu kuanzishwa kwake ambapo Maelfu ya Wanachama wa Chama hicho wameujaza uwanja wa Furahisha jijini Mwanza huku Askari wa jeshi la polisi wakionekana wakiwa maeneo ya uwanja huo ili kuimarisha ulinzi kwa wanachama.
Chanzo - EATV
Social Plugin