Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako,akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo lililofanyika leo Januari 10,2023 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Prof.Jamal Katundu,,akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo lililofanyika leo Januari 10,2023 jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako,wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo lililofanyika leo Januari 10,2023 jijini Dodoma.
.........................
Na Mwandishi Wetu, DODOMA Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako, amelitaka Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo kutoa maoni yanayoendana na mahitaji ya sasa kwenye Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2023. Prof.Ndalichako ametoa kauli hiyo leo Januari 10, 2023 alipokuwa akifungua mkutano wa Baraza hilo jijini Dodoma ambao pamoja na mambo mengine unajadili na kutoa maoni kuhusu sera hiyo. Amesema vijana ndiyo nguzo ya maendeleo ya taifa na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na mambo mengine jukumu lake kubwa ni kusimamia masuala ya vijana nchini. “Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2021 inaonesha kuwa kundi la vijana kati ya miaka 15 hadi 35 linajumuisha watu wapatao Milioni 20.73 sawa na asilimia 34.9 ya watu wote. Hili ni kundi muhimu katika kuleta maendeleo ya nchi yetu, vijana wanapaswa kujengewa misingi ya kulinda amani, umoja na kuendeleza mshikamano katika taifa letu,”amesema.
Aidha, amesema maandalizi ya kuandaa Sera ya Maendeleo ya Vijana bado yanaendelea na hatua kadhaa zimeshakamilika ikiwa pamoja na kufanya tathmini ya Sera ya mwaka 2007, kuandaa rasimu ya Sera ya Mwaka 2023,kuandaa rasimu ya mkakati wa utekelezaji na kupata maoni ya Menejimenti na Wakurugenzi wa sera na mipango wa Wizara.
Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya teknolojia na utandawazi, Prof.Ndalichako amesema mfumo wa maisha duniani umebadilika sana ikiwemo makuzi na tabia ya vijana.
“Tuangalie ni kwa namna gani vijana wetu watanufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.Ni namna gani wanaweza kutumia maendeleo ya Teknolojia ya habari na mawasiliano kama fursa ya kuwapatia ajira na kipato,”amesema.
Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prof.Jamal Katundu, amemhakikishia Waziri Ndalichako kuwa sera hiyo itakamilika ili itumike kwa maendeleo ya vijana nchini.
Social Plugin