Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SENYAMULE AONGOZA UPANDAJI MITI BONDE LA MZAKWE


***********************

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameongoza zoezi la upandaji miti katika eneo la chanzo cha maji cha bonde la Mzakwe zoezi ambalo ni muendelezo wa kampeni ya upandaji miti ngazi ya Mkoa iliyozinduliwa rasmi Desemba 31 kwa kupanda miti kwenye eneo la chanzo cha maji cha DUWASA kilichopo eneo la Ihumwa vijijini.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mhe. Senyamule amewataka wasimamizi wa Bonde la Wawi-Ruvu, wadau wa mazingira na wananchi kulipa bonde hilo usimamizi madhubutu bila kusukumwa kwani kila mmoja anapaswa kutambua wajibu wake juu ya kulilinda eneo hilo la hifadhi kutokana na umuhimu wake.

“Tuna imani kuwa utafiti wa kutosha ulikwishafanyika hapa hivyo tutaona miti itakayopandwa ikikua kwani hauwezi kupanda miti eneo ambalo halijafanyiwa utafiti wowote ni matumaini yangu kuwa kama utafiti ulifanyika kweli, basi tutaona miti ikikua vizuri na sio kufa” Amesema Mhe. Senyamule.

Ametoa msisitizo kwa wasimamizi wa eneo hilo kuhakikisha wanalitunza eneo la bonde la Mzakwe ili kupoteza historia mbaya iliyowahi kutokea miaka ya nyuma ya miti kutoota katika eneo hilo, miti kuungua moto na uvamizi wa wananchi kwa kuweka makazi katika vyanzo vya maji na kusababisha uharibifu wa mazingira.

“Tuna imani kubwa miti hii mtaitunza, itakua na kupoteza historia yote ambayo ilitokea katika bonde hili la Mzakwe. Ni wajibu wetu kutunza vyanzo vya maji kwa ajili ya matumizi ya maeneo mbalimbali. Sitatamani kuona uzembe wowote ambao utatokea wa kufanya miti hii isikue, nitoe onyo kwa wananchi ambao ni chanzo cha uharibifu wa miti hii kwa kuchoma moto na kuleta mifugo kwenye hifadhi kuwa ni kinyume cha kisheria na tutawachukulia hatua” Ameongeza Mhe. Senyamule.

Naye Bi. Feliciana Mpanda ambaye ni Afisa Kidaki cha Maji Wami-Ruvu, amesema chanzo hiki ni muhimu kwakuwa kinategemewa kuzalisha maji takribani lita Milioni131 yatakayotumiwa na Jiji la Dodoma licha ya changamoto zinazolikabili bonde hili. Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uingizaji wa mifugo na uchomaji moto unaofanywa na wananchi wanaozunguka bonde hilo na kutoa rai kwa jamii ukabililiana na changamoto hizi ili kulilinda bonde.

Vilevile, Afisa wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Bw. Frank Chombo, ameainisha aina 4 ya miti inatakayopandwa katika eneo hilo kulingana na tafiti za udongo zilizofanyika kwenye eneo hili na kuhimiza wananchi kufika kwenye bustani za Wakala wa Misitu Tanzania kote nchini kuchukua miche kwakuwa inapatikana kwa wingi. Kwa wakazi wa Dodoma, amesema bustani zipo maili mbili na eneo la Ikowa katika Wilaya ya Chamwino, pia wana miche zaidi ya Million 1 inayogawiwa bure.

Takriban miti 5,300 imepandwa katika bonde la Mzakwe katika kipindi cha mwezi mmoja na kampeni hii ni endelevu na lengo ni kupanda miti 40,000 ndani ya miaka minne.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com