Na Mwandishi Wetu.
KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ili kuifanya kuwa na mazingira bora zaidi ya utoaji wa taaluma ya sanaa na utamaduni.
Hayo ameyasema Januari 25, 2023 alipotembelea Taasisi Wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani katika ziara ya kukagua ukarabati wa miundombini na vifaa mbalimbali vya kufundishia na kijifunzia vilivyopatikana kwa fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali kila mwaka.
Dkt. Abbasi amesema Serikali itandelea kuongeza upatikanaji wa fedha za maendeleo ili kuhakikisha mazingira ya chuo yanaimarika kwa kukarabati miundombinu pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kujifunzia na kufundishia.
"Serikali itaendelea kutimiza ahadi yake ili kuifanya TaSUBa iendelee kua Chuo bora zaidi cha mafunzo ya sanaa na utamaduni Afrika na Duniani," amesema Dkt. Abbasi.
Amesema changamoto haziwezi kwisha kwa mara moja lakini TaSUBa imekua ikienda juu kila mwaka na kuongeza tija kwa sababu Serikali ina matashi mema kwa Taasisi na wananchi wake wote kwa ujumla.
Ameitaka TaSUBa kuendelea kubuni miradi mipya yenye tija kwa lengo la kukuza Chuo na Serikali itaendelea kutoa fedha.
"Sekta hii ndio Sekta shawishi inayochangia katika kuitangaza nchi kimataifa, mfano Brazil inafahamika kimataifa kupitia soka," amesema Dkt. Abbasi.
Katibu Mkuu Dkt. Abbasi amewataka watumishi wa TaSUBa kutumia elimu waliyonayo kubadili mazingira ya Chuo wakijua kwamba hakuna mwingine atakayekuja kubadilisha hali zao isipokua wao wenyewe kwa kuwa kama una elimu na huitumii ni kazi bure "Education without Application is Useless."
Aidha Dkt. Abbasi amewataka watumishi wa TaSUBa kuwa tayari kupokea mageuzi na kukubali kuacha kufanya kazi kwa mazoea jambo ambalo kwa kasi ya dunia ya sasa ni la msingi.
Sambamba na hayo Katibu Mkuu Dkt. Abbasi amemsimamisha kazi Naibu Mkuu wa Chuo TaSUBa Mipango Fedha na Utawala Bw. Emmanuel Bwire kwa tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya utumishi kazini na misingi ya utawala bora kwa nyakati tofauti alipokua akitumikia wadhifa wake huo. Bw. Bwire amesimamishwa kazi kuanzia January 25, 2023 ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo. Nao Mwenyekiti ya Bodi ya Ushauri ya Taasisi hio, Bw. George Yambesi pamoja na Mkuu wa Chuo Dkt. Herbert Makoye wamemshukuru Katibu Mkuu kwa ziara aliyoifanya TaSUBa na kuahidi kuyafanyia kazi yale yote aliyoelekeza na kuendelea kutimiza wajibu wao kadiri ya maelekezo ya viongozi na kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa mipango mbalimbali.
Social Plugin