SERIKALI YAKABIDHI VIBALI VYA UJENZI OFISI ZA TAASISI

Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene 

Na Dotto Kwilasa, DODOMA.

SERIKALI imekamilisha ratiba na mwongozo utakaowezesha Taasisi za Serikali ambazo bado zinaendelea kutekeleza majukumu yake Dar es Salaam kuweza kuhamishia shughuli zao Jijini Dodoma kwa awamu.

Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene amesema suala la kuhamia Dodoma sio la hiari bali ni takwa la kisheria na  kufuatia muongozo huo amezielekeza taasisi 42 zihamie Dodoma ndani ya mwaka huu wa fedha na kufafanua kuwa taasisi nyingine  36 zitahamia Dodoma katika mwaka ujao wa fedha.

Akizungumza Jijini hapa wakati akikabidhi vibali vya ujenzi wa ofisi za taasisi Waziri hiyo amesema  taasisi 19 zitahamia katika mwaka fedha  2024/25 wakati taasisi 27 zimeelekezwa, kwa kuzingatia aina ya majukumu zilizonazo, kuendelea kutekeleza majukumu yake Mkoani Dar es Salaam.

"Serikali ilikuwa na jumla ya taasisi 189 zilizokuwa zinatekeleza majukumu yake Jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, kutokana na zoezi la Serikali kuhamishia shughuli zake Jijini Dodoma,  taasisi 55 za serikali zimetekeleza maelekezo hayo kwa kuamua kujenga ofisi zake Dodoma,"amesema

Ameongeza kuwa "Hadi sasa taasisi 20 zimekamilisha ujenzi, taasisi 16 zinaendelea na hatua mbalimbali za ujenzi, taasisi nyingine 19 zipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi baada ya kupata vibali vya ujenzi kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Amebainisha kuwa majengo ya taasisi za serikali yanajengwa katika maeneo ya NCC Link, Medeli, Njedengwa Mtumba na Kikombo kwa kufuata mwongozo uliopo katika Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma.

Amesema ujenzi unaoendelea unategemewa kubadili mandhari ya Jiji la Dodoma pamoja na kupunguza changamoto ya ofisi na hivyo kuwezesha zoezi la serikali na taasisi zake kuhamia Dodoma kwa ufanisi zaidi.  

"Serikali inaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa majengo ya kudumu ya ofisi 26 za wizara yanayojengwa Katika ujenzi wa awamu ya pili,ujenzi huo umefikia wastani wa takriban asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika kabla ya Oktoba mwaka huu kwa gharama ya sh. bilioni 675;

Vilevile tunaendelea kuchukua hatua mahsusi za uboreshaji wa miundombinu ya miradi ya kimkakati Dodoma ikiwemo ujenzi wa uwanja Ndege Msalato utakaogharimu sh. billioni 165 ambao ujenzi wake umefikia asiimia 11, ujenzi wa barabara za mzunguko zenye urefu wa kilometa 112 na utagharimu sh. bilioni 221 ambao ujenzi umefikia asilimia 20, ujenzi wa Bwawa la Farkwa ambalo litazalisha maji mita za ujazo 130,000 kwa siku na kugharimu bilioni 325,"amesema

Ameongeza kuwa”Serikali inaendelea na  ujenzi wa mtandao wa maji kutoka Bwawa la Mtera hadi Dodoma utakaozalisha mita za ujazo 128,000 kwa siku, uboreshaji wa barabara za mtandao wa lami katika Jiji la Dodoma na ujenzi wa reli itakayozunguka Jiji la Dodoma ili kurahisisha huduma za usafirishaji na kupunguza msongamano.

Amesema taasisi zote zilizoelekezwa kuhamia Dodoma kwa mujibu wa ratiba zihakikishe zinatekeleza maagizo hayo na Makatibu Wakuu wa Wizara husika wahakikishe wanasimamia mpango kazi wa utekelezaji wake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post