SERIKALI YATOA TAMKO SUALA LA USHOGA SHULENI

Waziri wa elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda.

Na Dotto Kwilasa,DODOMA.

SERIKALI imesema inafuatilia kwa karibu taarifa zilizotolewa hivi karibuni na vyombo vya habari kuhusu shule ambazo zinafundisha wanafunzi masuala ya ushoga jambo ambalo ni kinyume na mitaala ya elimu hapa nchini.


Hatua hiyo imekuja kufuatia hivi karibuni chombo kimoja cha habari nchini kuripoti tukio la wanafunzi kulawitiana mkoani Kilimanjaro kinyume na taratibu za elimu zinavyotaka na kwenda kinyume na mila na desturi za Mtanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Waziri wa elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kutokana na hali hiyo tayari Serikali imewapeleka Kamishina wa Elimu, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora pamoja na Mwanasheria wa Wizara kufuatilia jambo hilo ili kuwabaini waliohusika.

"Kwa sasa hivi timu hiyo inapitia hizo shule na kupata taarifa lakini pia tumemuomba mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro kushirikiana na timu hiyo pamoja na kuwasaidia sehemu ambayo ina masuala jinai ili polisi wachukue hatua,"amesema.


“Tunatarajia kwamba hao walioenda wataleta taarifa kamili na sisi tuko tayari kuchukua hatua stahiki kudhibiti mambo hayo, zaidi ya hayo kwa kuwa suala hili limetokea eneo moja basi tunajua kunaweza kukawa na taarifa kwenye maeneo mengine,"amesisitiza

Pamoja na hayo Waziri huyo mwenye dhamana ya elimu nchini amesema kupitia wizara hiyo Katibu Mkuu atatoa namba ambayo mtu yeyote mwenye taarifa kama hiyo katika shule yeyote iwe ya umma au binafsi au vyuo vyovyote hapa nchini aweze kuwasiliana naye moja kwa moja .


“Tutafuatilia kwa nchi nzima, tunaongeza umakini kwa kufuatilia mambo haya kwa sababu tunajua yanaweza kuchafua taswira ya elimu,yanaharibu vijana wetu na hata wazazi kukosa imani na shule”, amesema.

Kwa kutilia mkazo suala hilo, Prof. Mkenda amesema walifanya mkutano ambao ulikuwa chini ya Mwenyekiti Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu George Simbachawene,Waziri wa Maendeleo ya jamii Dk. Dorothy Gwajima na Waziri wa TAMISEMI pamoja na makatibu wakuu kwa ajili ya kuangalia namna ya kudhibiti mambo hayo.

“Suala hili ni nyeti na lazima tulishughulikie kwa umakini mkubwa,tumeanza mkakati wa kitaifa wa kuangalia namna ya kudhibiti tatizo hili kuanzia majumbani, njiani na maeneo mbalimbali ,"amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post