Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akizungumza kabla ya kuanza kwa mafunzo kuhusu Programu ya TAKUKURU RAFIKI yaliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa Wajumbe wa Kamati yake jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifungua mafunzo ya Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) yaliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) jijini Dodoma.
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (aliyesimama) wakati naibu waziri huyo alipokuwa akifungua mafunzo ya Programu ya TAKUKURU RAFIKI yaliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) jijini Dodoma.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kufungua mafunzo ya Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) yaliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) jijini Dodoma.
Afisa Uchunguzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. John Shija (Wa kwanza kulia) akiwasilisha mada kuhusu Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) wakati wa mafunzo yaliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa wajumbe wa kamati hiyo jijini Dodoma.
Mjumbe wa Kamati ya USEMI ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Makete, Mhe. Festo Sanga akichangia hoja wakati wa mafunzo ya Programu ya TAKUKURU RAFIKI, yaliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uelewa wa programu hiyo wajumbe wa kamati ya USEMI.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI), Mhe. Abdallah Chaurembo akiteta jambo na Makamu Mwenyekiti wake, Mhe, Denis Londo walipokuwa kwenye mafunzo ya Programu ya TAKUKURU RAFIKI yaliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa Wajumbe wa Kamati hiyo ya USEMI jijini Dodoma.
************************
Na. Veronica Mwafisi-Dodoma Tarehe 22 Januari, 2023.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoa mafunzo kwa watendaji wa kata kuhusu utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU RAFIKI ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa nchini, ambavyo vimekuwa ni kikwazo cha maendeleo katika taifa.
Mhe. Chaurembo ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma, wakati Kamati yake ya USEMI ikipatiwa mafunzo na TAKUKURU kuhusu Programu ya TAKUKURU RAFIKI, ambayo yaliyolenga kuwajengea uelewa wa program hiyo wajumbe wa kamati hiyo ili washirikiane na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa.
Mhe. Chaurembo amesema, moja ya jukumu la Watendaji Kata ni kuwasaidia Wakurugenzi na Watendaji wengine kuleta maendeleo katika ngazi ya Kata, hivyo wakiielewa vema programu ya TAKUKURU RAFIKI itawasaidia kwenye eneo la usimamizi wa miradi katika sekta kipaumbele za afya, maji, elimu, kilimo, ardhi na miundombinu.
“TAKUKURU ni wajibu wenu kuhakikisha Watendaji wa Kata wanapatiwa mafunzo ya Programu ya TAKUKURU RAFIKI ili waweze kuwaunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa,” Mhe. Chaurembo amesisitiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema TAKUKURU RAFIKI ni programu iliyotokana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliielekeza TAKUKURU kuandaa programu itakayoiwezesha kuzuia vitendo rushwa badala ya kupambana navyo.
Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya USEMI ya kutoa elimu kwa Watendaji wa Kata kuhusu Programu ya TAKUKURU RAFIKI, Mhe. Ndejembi amesema TAKUKURU itaenda kwenye ngazi ya Kata kutoa elimu hiyo kwa watendaji hao ikiwa ni pamoja na wananchi ili kila mwananchi aweze kuwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.
Naye, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye amesema taasisi yake ina ari, azma na nia ya kuhakikisha kwamba rushwa inatokomezwa nchini Tanzania kupitia Programu ya TAKUKURU RAFIKI.
Akizungumzia mwitikio wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa, Bi. Mwakalyelye amesema asilimia 92 ya wananchi wameonesha utayari wa kushiriki mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo katika taifa, hivyo Programu ya TAKUKURU RAFIKI itatumika kikamilifu kuitokomeza rushwa.
Aidha, Bi. Mwakalyelye ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) kwa maelekezo na maoni iliyoyatoa na kuahidi kuyafanyia kazi ili TAKUKURU itekeleza jukumu lake la msingi la kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa nchini.
Programu ya TAKUKURU RAFIKI ilianzishwa kwa lengo la kuongeza ushiriki wa mwananchi na wadau katika kukabiliana na tatizo la rushwa kwenye eneo la utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.