Dotto Kwilasa, DODOMA.
TANZANIA imejipanga kuwa kitovu cha biashara mtandao inayovuka mikapa barani Afrika kwa kupanua wigo wa kasi ya ukuaji wa Teknolojia na kuwa sekta tegemezi katika kukuza uchumi.
Hayo yameelezwa Jijini hapa na Waziri wa Habari, mawasiliano na Teknolojia ya habari Nape Nnauye wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya posta Afrika na kueleza kuwa umuhimu wa Posta unawezesha umahiri wa biashara kidigitali.
Amesema ili kupanua wigo wa biashara mtandao Serikali imeweka mifumo ya sera,Sheria na usimamizi Wenye umakini juu ya biashara mtandao na kuendeleza uwekezaji wake kwa viwango vya juu.
Waziri huyo pia amesema kwa kuwa Serikali inatambua biashara mtandao ni kipaumbele kwa nchi za Afrika itawekeza zaidi katika usalama,amani,urahisi na ufanisi mtandaoni ili kuchochoea mageuzi ya Afrika kidigitali.
"Tunatambua umuhimu wa Posta hivyo sisi kama Serikali tumejipanga kukamilisha ujenzi jengo la Posta Afrika lenye makao yake makuu Jijini Arusha,hivyo niwaombe nchi wanachama wa Posta Afrika kutekeleza kwa wakati maazimio yaliyowekwa"amesema
Katika kutekeleza yote hayo ,Mkurugenzi wa Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA)Jabir Bakar Kuwe amesema mamlaka hiyo itaendelea kuweka mazingira ya kuvutia kibiashara ili kukabiliana na soko la kimataifa.
Amesema wao kama wadau wa Posta wamejipanga kuongeza wigo wa Teknolojia kuendana na viwango vya kimataifa ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto na vikwazo vilivyopo mipakani.
"Tunawezesha upatikanaji wa bidhaa na kuwezesha wananchi kununua bidhaa hadi mlaji ,lengo letu kubwa ni kuongeza mngororo wa usambazaji bidhaa kidigitali,"amesisitiza
Naye Kaimu Posta master mkuu, Ferdinand Kabyemelwa amesema kuwa Posta imedhamiria kujiendesha kibiashara ikiwemo kutoa nafasi ya kuwa kitovu cha biashara ya mtandao ambayo imekuwa kipaumbele cha Afrika yote, kama ilivyosisitizwa kwenye azimio la Afrika la mwaka 2020 kuhusu Kuibadili Afrika Kidijitali.
“Azimio hilo linataka kuwepo Soko Moja ya Kidijitali Afrika ifikapo mwaka 2030, ambapo hapatakuwa na mipaka ya watu, bidhaa,tutaendeleza uwekaji na uendeshaji wa miundombinu katika maeneo yote yanayohusiana na biashara mtandao ,"amesema