Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIPODOZI VYATEKETEZWA


SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza tani 20 ya bidhaa hafifu na bidhaa duni ambazo hazikidhi matakwa ya viwango kwa mujibu wa sheria ya viwango zenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 400.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 14, 2023 Kisarawe mkoani Pwani, Kaimu Meneja wa Kanda ya Mashariki (TBS) Bw.Francis Mapunda, amesema bidhaa hizo zilikamatwa kwenye masoko yaliyopo kwenye mikoa ya Dar es Salaam,Morogoro pamoja na Pwani wakati wa ukaguzi wa kushtukiza.

Amesema bidhaa ambazo wameziteketeza ni pamoja na vipodozi, kofia za pikipiki na aina zingine za bidhaa ikiwemo vyakula vilivyoisha muda wa matumizi ambavyo vilikuwa vinaendelea kuuzwa katika maduka yaliyopo kwenye masoko ya mikoa hiyo.

"Tunawaasa wafanyabiashara kuacha kuuza bidhaa ambazo hazikidhi matakwa ya viwango, kuacha kuuza vipodozi ambavyo vimezuiliwa na kuacha kuuza bidhaa ambazo zimeisha muda wa matumizi kwa kuwa wakaguzi wetu (TBS) muda wote wapo kazini na tunashirikiana na wananchi na vyombo vingine vya dola katika kuhakikisha bidhaa ambazo ziko kwenye soko ni zile zinazokidhi viwango". Amesema Bw.Mapunda.

Amesema zoezi la uteketezaji wamelianza Juni 11 na kuhitimisha leo ambapo zoezi linaenda vizuri katika kuhakikisha bidhaa zote hizo zinateketezwa kwa mujibu wa sheria ya Viwango.

Aidha amesema lengo la TBS ni kukuza biashara nchini lakini wanataka watu wafanye biashara ambazo ni za halali na haki bila kuleta athari ya afya kwa mtumiaji wa bidhaa.

Kwa upande wake Mkaguzi Mwandamizi TBS Kanda ya Mashariki, Bw. Aron Zala amesema madhara ya kutumia bidhaa za vipodozi vilivyopigwa marufuku ni pamoja na kuongezeka kwa saratani, matatizo mengine ya kiafya pamoja na kuathirika kiuchumi.

Amewaasa wananchi kuwa makini na ununuaji wa bidhaa sokoni ikiwemo chakula kuangalia tarehe ya za kutengenezwa na tarehe za kuisha muda wake lakini vilevile na kuangalia kwenye mitandao ya kijamii bidhaa ambazo zimepigwa marufuku kwamba si salama kwa matumizi ya binadamu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com