WANUFAIKA MIRADI YA MFUKO ELIMU WAISHUKURU TEA

Jengo la Maabara ya Sayansi lililojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa katika Shule ya Sekondari Magwanjwa iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bahati Geuzye (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Anna Mbogo (wa kwanza kushoto) wakati wa ziara ya kutembelea miradi iliyofadhiliwa na Mfuko wa Elimu wa Taifa katika Wilaya hiyo Mkoani Manyara
Baadhi ya matundu ya vyoo yaliyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa katika Shule ya Sekondari Dareda iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara.
Vyumba vitatu vya madarasa vilivyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa katika Shule ya Sekondari Sokoni II iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Mkoani Arusha.Vyumba vitatu vya madarasa vilivyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa katika Shule ya Msingi Kaloleni katika jiji la Arusha.

**********************

Wanufaika wa miradi ya Mfuko wa Elimu katika Mikoa ya Arusha na Manyara wameipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kuboresha miundombinu ya elimu katika maeneo yao hali ambayo wamesema imechangia kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia katika maeneo hayo.

Pongezi hizo zilitolewa kwa TEA wakati wa ziara ya kikazi ya Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye kwenye miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Elimu katika Mikoa ya Arusha na Manyara ambapo alitembelea miradi ya ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya Sekondari Sokoni II na madarasa mengine matatu katika shule ya Msingi Kaloleni zote za jijini Arusha.

Miradi mingine iliyotembelewa katika ziara hiyo ya siku tatu iliyofanyika mwezi Desemba mwishoni 2022 ni miradi ya ujenzi wa matundu 24 ya vyoo katika shule ya msingi ya Kaloleni Jijini Arusha, shule ya msingi Gidewari pamoja na shule ya sekondari Dareda zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TEA alitembelea ujenzi wa maabara ya sayansi katika shule ya sekondari Maganjwa ya Babati mkoani Manyara na mradi wa ufadhili wa wanafunzi wanofanya mafunzo ya utalii na ukarimu katika chuo cha VETA-Arusha yanayofadhiliwa na Taasisi ya Asilia Giving kupitia Mfuko wa Elimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Bi Anna Mbogo alisema, mradi wa maabara ya sayansi katika shule ya sekondari Maganjwa katika Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Babati utainua ufaulu wa masomo ya sayansi katika shule hiyo kwa kuwa utawezesha wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Seleman Msumi nae alisema, Mfuko wa Elimu umewezesha halmashauri yake kujenga madarasa matatu ya kisasa pamoja na kununua samani ambazo ni viti na meza hali iliyosaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika vyumba vya madarasa kwenye shule hiyo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TEA alisisitiza umuhimu wa shule zilizonufaika na ufadhili wa Mfuko wa Elimu kutunza vyema miundombinu walizopata ili zidumu na kunufaisha wanafunzi wengi zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA alitembelea jumla ya miradi sita ya ujenzi wa miundombinu ya elimu yenye thamani ya shilingi Milioni 360 fedha ambazo zimetolewa na Mfuko wa Elimu wa Taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post