Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKENDA-VYUO VYA UALIMU VINA SEHEMU MUHIMU KATIKA KUTEKELEZA MITAALA MIPYA NCHINI


******** 

Serikali imesema katika mageuzi makubwa ya elimu yanayotarajiwa kufanywa nchini vyuo vya ualimu vina sehemu muhimu katika kutekeleza mitaala mipya chini ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 iliyoboreshwa. 

Akizungumza Mkoani Kilimanjaro mara baada ya kukagua miundombinu ya Chuo cha Ualimu Marangu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema kazi kubwa iliyopo sasa ni kupitia vyuo vyote ili kuona namna vitakavyojipanga kwa ajili ya kutekeleza mitaala hiyo. 

Ameongeza kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 imefanyiwa mapitio makubwa na itatolewa ikiwa ni toleo la 2023 la Sera hiyo kwa sababu kuna mambo makubwa ndani yake ambayo hayakuwa yametekelezwa ambayo yamepitiwa na kufanyiwa mabadiliko kidogo. 

"Mnajua kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tuna mageuzi makubwa katika elimu, kazi tumemaliza tunasubiri taratibu za ndani za serikali, tutatoa mitaala mipya na toleo la la mwaka 2023 la Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014" amesema Prof. Mkenda 

Ameongeza kuwa kuna vyuo vya ualimu vya serikali 35 ukiondoa vingine vya Taasisi mbalimbali na sekta binafsi ambapo kwa sasa vina takribani wanafunzi 22,000 . 

Waziri huyo amesema sasa ni wakati wa kufikiria na kufanya maamuzi magumu ya kuchagua kati ya kuzalisha kwa wingi walimu ama kuangalia ubora wa elimu inayotolewa kwa kuwa na idadi ya wanafunzi itakayowezesha kuwafundisha na kuhakikisha wanakuwa mahiri. 

Wakati huo huo, Profesa Mkenda ameagiza kufuatwa kwa kalenda ya Masomo ya Mwaka 2023 iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Kamishna wa Elimu. 

Amesema kuna baadhi ya mikoa imeweka mikakati ya wanafunzi kujifunza lugha kabla ya kuanza masomo, amewataka pamoja na mikakati hiyo kuhakikisha kalenda ya masomo inafuatwa ili kuwezesha wanafunzi kukamilisha mzunguko wa masomo 

Naye Mkuu wa Chuo cha Ualomu Marangu Dkt. Colonel Chambulila amemweleza Waziri wa Elimu kuwa Chuo hicho kilifanyiwa ukarabati mkubwa wa miundombinu kupitia Mradi wa EP4R kwa gharama ya zaidi ya shilingi Milioni 66 ambao ulihusisha ukarabati wa miundombinu ya mabweni, madarasa, maabara, jiko na maktaba. 

Dkt. Chambulila ameongeza kuwa kwa mwaka wa masomo 2022/23 Chuo hicho kimedahili Wanachuo 1,081na kufanya upungufu wa wanafunzi 19 tu ili kufikisha uwezo wa kudahili wa Chuo. Ameongeza kuwa idadi hiyo hajawahi kutokea hapo kabla .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com