Familia moja katika kijiji cha Miyare Karadolo huko Ugenya Magharibi, Siaya, inaomboleza kumpoteza mama yao ambaye aliumwa na nyuki hadi kufa.
Patricia Atieno Owino aliumwa mara kadhaa baada ya trekta iliyokodishwa kulima shamba lake kugonga mzinga wa nyuki kwa bahati mbaya.
Inasemekana kwamba nyuki hao walipandwa na mori na kuanza kumshambulia mtu yeyote aliyekuwa karibu na ni mbio tu ingemuokoa. Billian Ojiwa, mjukuu wa marehemu, aliripoti kuwa nyanyake hakuweza kukimbia kutoka eneo la tukio na hivyo basi akakumbana na mauti.
"Kila mtu alifanikiwa kutoroka eneo la tukio baada ya trekta kugonga mzinga wa nyuki hao na kuanza kuwashambulia watu," Ojiwa aliambia Nairobi News.
Alipelekwa katika hospitali moja huko kaunti ya Siaya, ambapo alikata roho alipokuwa akipokea matibabu ya kuumwa.
Nyuki wa asali wa Kiafrika wanajulikana kuua mamalia wakubwa na hata wanadamu, haswa watoto na wazee, ambao wana shida kutoroka.
Ojiwa alifichua kwamba familia ilikuwa na uchungu mwingi kwani kifo cha ajuza huyo kilitokea wiki tatu tu baada ya kumzika mtoto wa nyanyake.
Mwili wa mjombake ulikuwa Marekani kwa takriban miezi miwili walipokuwa wakitafuta fedha za kumsafirisha hadi nyumbani kwa mazishi .
Aliongeza kuwa wawili hao walikuwa nguzo ya familia yao ambao walihakikisha wanapata mahitaji yao hata nyakati zikiwa ngumu.
"Bibi yangu ameenda wiki chache tu baada ya mjomba wetu pia kufariki dunia Wawili hao wamekuwa nguzo kuu katika familia na pia walihakikisha kwamba mambo kila mtu yuko sawa nyumbani," aliongeza.