Picha zikionesha wanafunzi wakiwa chini
Picha halisi katika shule ya sekondari Sinde
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Wakili Triphonia Kisiga, amesema Mwalimu wa kujitolea katika shule ya sekondari Sinde, Evarist Chonya, aliyesambaza picha za uongo za wanafunzi wakiwa wamekaa chini amesimamishwa na kwamba kwa kuwa sio mwajiriwa atafukuzwa kabisa.
Picha hizo zimesambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ikielezwa kuwa wanafunzi hao wanakaa chini kutokana na uhaba wa madawati unaoikabili shule hiyo na kuibua taharuki kwa jamii.
Imeelezwa kuwa mwishoni mwa wiki madawati yote ya shule hiyo yalitolewa nje ya vyumba kwa ajili ya kuyaandika majina ya wanafunzi ili kila mwanafunzi awe na dawati lake ambalo atakuwa analitumia na kulitunza mpaka atakapohitimu kidato cha nne.
Na kwamba wakati shughuli hiyo ikiendelea mwalimu huyo aliwarejesha darasani baadhi ya wanafunzi na kuwaamuru wakae chini kisha akawapiga picha kwa nia ambayo haijulikani.
Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Anathalia Luwungo amesema shule hiyo ina wanafunzi 1300 kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne ambao wote wanakaa kwenye madawati na hakuna mwanafunzi hata mmoja ambaye anakaa chini kama ambavyo picha hizo zinaeleza.
Chanzo - EATV
Social Plugin