Na Halima Khoya, Malunde 1 blog
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Shinyanga imetambulisha Programu ya “TAKUKURU-Rafiki” kwa Madiwani na wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ili kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau katika kutokomeza tatizo la rushwa katika utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akitambulisha programu hiyo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Februari 10 2023 Kata ya Iselamagazi Halmashauri ya Wilaya ya shinyanga, Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Helga Mfuruki amesema programu hiyo inaakisi maana ya neno “Rafiki”kwa kubeba dhana ya kuwa karibu na ushirikiano na wananchi na wadau.
Amesema Programu hiyo itatekelezwa kwa kuwa na vikao ngazi ya kata ili kutambua kero zilizopo kwenye utoaji au upokeaji wa huduma mbalimbali.
“Baada ya kutatua kero hizo zilizoachwa pasipo kutatuliwa au kupatiwa ufumbuzi zinaweza kusababisha kutokea kwa vitendo vya rushwa, washiriki wa vikao hivyo wakiwamo wananchi,viongozi wa kisiasa, watendaji wa Serikali na Wazabuni watashirikiana kutatua kero hizo au kuweka mikakati jinsi ya kuzitatua kwa pamoja”, ameeleza Mfuruki.
Mfuruki amesema programu ya “TAKUKURU-Rafiki” itachangia kukuza ustawi wa utawala bora kwa kuzuia vitendo vya rushwa visitokee katika utoaji wa huduma kwa umma au utekelezaji wa miradi ya maendeleo sambamba na kuokoa fedha za umma kwa kujengwa au kutekelezwa miradi bora, endelevu na inayokidhi thamani ya fedha iliyotumika.
Ameongeza kuwa TAKUKURU-Rafiki itasaidia kuongeza uzingatiaji wa misingi ya utawala bora, ushirikiano wa kila mwananchi na wadau katika mapambano dhidi ya Rushwa na kuaminika kwa serikali kwa wananchi inayowahudumia.
“TAKUKURU imekuwa karibu nawe mwananchi na mdau ili katika namna rafiki tushirikiane kuzuia vitendo vya rushwa visitokee katika utoaji wa huduma kwa umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia program hii ya “TAKUKURU-Rafiki” usikae mbali,tushirikiane ili kwa pamoja tuijenge Tanzania",amesema.