Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATUMISHI HOUSING YAVUKA LENGO UKUSANYAJI MAPATO





Na Dotto Kwilasa, DODOMA.

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Watumishi Housing Investment (WHI), Dokta Fred Msemwa amesema kupitia Mfuko wa Faida fund ambao unatumia mfumo wa malipo ya Serikali wamevuka lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 12.9 huku matarajio yao yakiwa ni kukusanya bilioni 7.8 ikiwa ni ndani ya miezi miwili tangu kuanzishwa kwake.


Hayo ameyasema jijini Dodoma wakati alipokuwa akieleza utekelezaji wa majukumu ya mfuko huo ambapo alisema kuwa wamefanikiwa kuwanufaisha watanzania kuongeza kipato kupitia uwekezaji wa pamoja katika Faida Fund.


Amesema kuwa makusanyo hayo ya Mfuko ni katika kipindi cha Novemba mwaka jana na mpaka kufikia Februari 9 walikuwa na bil.14, na kusema kuwa fedha hizo wameziwekeza katika masoko ya fedha ikiwemo mabenki na Serikali ambapo watanzania zaidi ya 4000 wamejiunga.


"Kwa sasa Watanzania 80000 ndio wanaoshiriki katika uwekezaji wa pamoja wa soko la fedha, hivyo nawashauri watanzania kujitokeza kujiunga na mfuko huu ambao utawawezesha kufikia malengo, kujiletea maendeleo na kujikwamua kiuchumi”, amesema.


Akizungumzia uendeshaji wa Mfuko huo, Mkurugenzi huyo amesema kuwa Faida Fund unafanya kazi kwa njia ya kuuza vipande, ambapo bei ya kipande ilikuwa sh 100, mpaka sasa thamani ya kipande imefikia sh 101.1, hivyo thamani ya vipande imeendelea kukua.


“ Watumishi Houseng ndio wanaonunua vipande kutoka kwa wawekezaji ambao ni wanachama wa Mfuko huo watakaokuwa na uhitaji wa kuuza vipande vyao ili wapate Fedha”, amesema.


Dk. Msemwa ametaja faida ya kuwekeza kwenye Mfuko huo kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kuwekeza katika masomo ya Fedha bila kulazimika kufuata mlolongo mrefu ikiwemo kwenda kwa madalali, uwekezaji hufanyika kwa njia simu hivyo kuokoa muda na kuwa na usalama wa fedha na kupata unafuu na kuwekeza bila tozo huku uwekezaji wako ukitambulika kwa kasi kubwa.


Amesema uwekezaji unaweza ukautumia kama dhamana pale utakapohitaji mkopo wa Benki ili kujiongeza zaidi kiuchumi na Mfuko wa faida fund ni endelevu na unalengwa sekta zote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com