BALOZI WA DENMARK AIPONGEZA BENKI YA CRDB KWA MATOKEO MAZURI YA FEDHA

Balozi wa Denmark nchini, Mette Nørgaard Dissing-Spandet (wapili kushoto) katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (wakwanza kushoto), Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori, na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati walipomtembelea ofisini kwake kujadili uwekezaji wa DANIDA ndani ya benki hiyo na Mkakati mpya wa Miaka Mitano wa Biashara wa Benki ya CRDB wa 2023/2028.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wakwanza kulia) akimwelezea Balozi wa Denmark nchini, Mette Nørgaard Dissing-Spandet (wapili kushoto) juu ya Mkakati mpya wa Miaka Mitano wa Biashara wa Benki ya CRDB wa 2023/2028 wakati ujumbe wa Benki hiyo ulipotembelea katika Ubalozi wa Denmark kujadili mafanikio ya uwekezaji wa DANIDA ndani ya benki hiyo. Ujumbe huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (wapili kushoto), pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (hayupo pichani), Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa (watatu kushoto), na Katibu wa Kampuni Benki ya CRDB, John Rugambo.

Na Mwandishi Wetu

Uongozi wa Benki ya CRDB kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Abdulmajid Nsekela umekutana na Balozi wa Denmark nchini, Mh. Mette Nørgaard Dissing-Spandet kujadili uhusiano baina ya Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA) na benki hiyo.

Hakuna wakati mzuri wa kujadili uhusiano huo wa kihistoria kama kipindi hiki ambacho benki hiyo kinara wa utoaji huduma za kifedha nchini, imetoka kupata faida kubwa kwa mwaka uliopita.

Ikiivunja rekodi yake yenyewe iliyoiweka kwa mwaka 2021 ya faida baada ya kodi ya takriban Sh268 bilioni na kufikia faida ya Sh353 bilioni kwa mwaka 2022.

Mafanikio hayo yanaelezwa kutokana na jitihada za makusudi za benki hiyo kukuza vyanzo vya mapato yasiyotokana na riba ambapo yaliongezeka kwa asilimia 13 mwaka hadi mwaka na kufikia kiasi cha Sh400 bilioni kutoka Sh354 bilioni.

Nsekela, akifafanua rekodi hiyo, alisema imechagiwa na ongezeko la ufanyaji miamala ya fedha hususan kupitia njia za kidijitali.

Kiujumla, wanahisa wa benki hii, DANIDA akiwa mmojawapo akishirikiana na Serikali ya Tanzania, wanaendelea kuona fahari ya kuwa sehemu ya uwekezaji wa benki inayofanya vizuri kwa kuwa wana uhakika gawio lao litaongezeka maradufu.

Balozi Dissing-Spandet akizungumza na viongozi wa Benki ya CRDB alisema amefurahishwa na matokeo mazuri ya Benki ya CRDB kwa 2022 na ni kiashiria kizuri kwa matokeo yajayo.

Historia ya DANIDA na Benki ya CRDB

Uhusiano wa DANIDA na Benki ya CRDB haujaanza leo, mizizi yake ilipandwa kupitia uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Denmark.

Tanzania imekuwa mnufaika wa misaada ya kimaendeleo kutoka kwa Denmark kupitia DANIDA kwa miongo kadhaa iliyopita ikitekeleza miradi ya afya, uchumi, utafiti, ujasiriamali nk.

Wakati Benki ya CRDB ikijulikana kama Cooperative Rural Development Bank, ilipitia nyakati ngumu kiasi cha kushindwa kujiendesha hatua iliyopelekea Serikali kuiomba DANIDA kupitia wake Mfuko wa Uwekezaji wa Denmark (DIF) kuinasua benki hiyo.

Kuingia kwa DIF kama mwekezaji kuliweza kuleta mageuzi katika benki hiyo ambayo ilipelekea kuzaliwa upya kama Benki ya CRDB. Miaka kadhaa baadaye Benki ya CRDB ilifikia hadhi yakuweza kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Uwekezaji wa hisa na urudishaji kwa jamii

DIF ilianza kwa kuwekeza hisa 247,014 mwaka 2002 ambazo zimeongezeka na kufikia hisa 548,067,648 mwaka 2021 ambazo ni sawa na asilimia 21 ya hisa zote za Benki ya CRDB.

Katika upande wa gawio, DIF na Serikali ya Tanzania, zilipata kiasi cha Sh247 milioni mwaka 2002 na Sh19.7 bilioni mwaka 2021.

Uhusiano huu wa aina yake baina ya DANIDA, Serikali na Benki ya CRDB umekuwa na maana kubwa katika kuifanya benki hii kuendelea kufanya vyema kila mwaka na kupata faida katika biashara yake.

Serikali ya Denmark imeendeleza ushirikiano wake na Benki ya CRDB na sasa imewekeza kupitia Mfuko wake wa Uwekezaji unaoitwa Investment Fund for Developing Countries (IFU), kwenye Kampuni tanzu ya CRDB Bank nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa kuwa DANIDA ni mdau wa maendeleo nchini, inaelezwa kuwa Denmark ilikuwa miongoni mwa waasisi wa Fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja (HBF) mwaka 1999 na imekuwa ikiendelea kuchangia katika mfuko huo. Kwa mwaka huo pekee, ilichangia kiasi cha DKK 60 milioni.

Kupitia mchango wake katika fedha za mifuko ya afya ya pamoja kwa bara na visiwani, Danida imekuwa ikitumia fedha zake za uwekezaji kusaidia kuboresha mifumo ya afya, ubora wa huduma za afya, huduma za afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana.

Kwa mantiki hiyo, ili DIF inayoshirikiana na Serikali, iweze kuendelea kusaidia upatikanaji wa huduma za afya katika jamii zenye uhitaji mkubwa inalazimika kutenga kiasi cha gawio litokanalo na faida ya uwekezaji wake kila mwaka kwa Benki ya CRDB kufanikisha jitihada hizo.

Kwa kuwa mfuko huo na mingine bado inategemea michango kutoka kwa wadau wa maendeleo, Benki ya CRDB inabaki kuwa tegemeo la wadau wengi ambao wanachangia katika mfuko huo kupitia gawio inaloligawa kila mwaka baada ya kuwekeza hisa zao.

Ni sahihi kusema kuwa benki hiyo imekuwa ikisaidia moja kwa moja katika HBF kupitia wanahisa wake wanaopata gawio kila mwaka, kwa mantiki hiyo, ina dhima kubwa ya kuendelea kuhakikisha inakuja na mikakati bora ya kuiwezesha benki kufanya vizuri kwa mwaka huu na inayofuata na wanahisa wake kuchangia zaidi.

Kwa mwaka wa fedha 2022/23, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kuwa wadau wa HBF walikubaliana kuchangia kiasi cha Sh98.1 bilioni kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.

“Fedha zinazoingizwa nchini kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za afya tunapenda ziingizwe kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja ili tuweke kushirikiana kufanya kazi pamoja na kupata matokea ya haraka kwa pamoja. Mapendekezo yetu wadau wengine wachangia kupitia mfuko huo kwani tumeona mafanikio makubwa" amefafanua Waziri Ummy Mwalimu.

Aidha Waziri Ummy Mwalimu amesema upo umuhimu kwa wadau wa maendeleo kuchanga fedha kwa pamoja na kuweka kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuzingatia Mifumo na taratibu za Serikali za kutoa fedha kwa ajili ya Huduma za Afya nchini pamoja na kuwekeza fedha kwenye maeneo ya vipaumbele vya Serikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post