Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADIWANI SHINYANGA DC, WAIOMBA SERIKALI KUKAMILISHA MIRADI YA AFYA YA MUDA MREFU


Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Shinyanga Simon Nicholas
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Shinyanga Simon Nicholas

Na Halima Khoya - Malunde 1 blog
Baadhi ya Madiwani  katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mkoani Shinyanga wameiomba serikali kukamilisha  ujenzi wa majengo ya hospitali yaliyokaa muda mrefu ili kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya.

Wakizungumza katika baraza la Madiwani lililofanyika leo Febuari 9 2023 katika ukumbi wa hospitali ya Halmashauri hiyo Mkoani Shinyanga ambapo wameiomba Halmashauri kutoa fedha ili kukamilisha majengo ya baadhi ya zahanati hizo.

Wakieleza jitihada zilizofanywa na wananchi ,Diwani wa Kata ya Samuye John Ngengeshi na diwani wa kata ya Tinde,Jafari Kanolo,wamesema kumekua na maboma ya zahanati ambayo hayajaanza kutoa huduma kwasababu ya uchache wa fedha ambazo hazijakidhi ujenzi huo na kwamba  wanaiomba Halmashauri kuwaunga mkono ili kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu.

"Kwa ujumla wananchi wa kata ya Tinde wanajitahidi sana kuchangia ujenzi wa miradi,kuna boma la zahanati lina miaka 10 hadi sasa hivi halijaanza kutumika kwasababu limesimama kwa muda mrefu bila kujengwa baada ya wananchi kutokuwa na fedha za kutosha,tunaiomba Halmashauri yetu katika makusanyo ya mapato ya ndani itusaidie", amesema Jafari.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Shinyanga Simon Nicholas, amesema kila taarifa ya kata zilizowasilishwa zimempongeza Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa wananchi wake kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika jamii hivyo kuwaomba madiwani wakasimamie miradi yote inayoendelea kwenye kata zao.

Nicholas amewataka viongozi wa mamlaka mbalimbali katika wilaya hiyo kutatua changamoto hizo  pind Serikali itakapotoa bajeti ya fedha kwa mwaka 2023/24 wapeleke katika miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na majengo yaliyokaa kwa muda mrefu bila kukamilika ujenzi wake.

"Pindi Serikali itakapoleta fedha tuzipeleke katika miradi yetu na kuweka fedha kwa ajili ya majengo yaliyokaa kwa muda mrefu", amesema 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com