Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi ILALA limewaasa vijana wa ulinzi shirikishi kuweka nadhili ya kuukataa uhalifu katika mitaa yao.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 22/02/2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala Dr. Debora D. Magiligimba ACP katika bwalo la Polisi Stakishari alipokutana na vijana wa ulinzi shirikishi katika wilaya ya Kipolisi Ukonga kwa ajili ya kuwajengea morali ya kazi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Akitoa maelekezo hayo Kamanda Dr. Magiligimba ACP aliwataka vijana hao kuwafichua watu wote ambao wamekuwa wakitenda/ kuhisiwa kutenda makosa ya jinai ili Jeshi la Polisi liweze kuwatambua na kuwaweka katika utaratibu wa uangalizi wa Polisi kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza matukio ya uhalifu katika mitaa yao.
Aidha, Kamanda Magiligimba aliwataka vijana wa ulinzi shirikishi kujipanga upya kwa kuhakikisha wanafanya utafiti wa kubaini ni muda gani ambao uhalifu unatendeka ili katika muda huo waanze kuingia kazini.
Amesema " sasa hivi wahalifu wamebadili muda wa kutenda uhalifu wao kwani wanajua kuwa kuanzia majira ya saa sita usiku kunakuwa na ulinzi shirikishi mtaani hivyo wao wamebadili muda na kuanza kufanya matukio yao mapema zaidi. Hivyo tunapaswa kuendana na upepo wao".
Kwa upande wake Mkuu wa ushirikishwaji wa jamii Mkoa wa Kipolisi Ilala R.M. Shemndolwa ACP amesema kuwa kwa sasa Mkoa wa Kipolisi Ilala umejipanga kuhakikisha vijana wote wa ulinzi shirikishi wanapata posho zao pamoja na stahiki mbalimbali kupitia mfumo mpya wa ukusanyaji wa michango hiyo ambapo kwasasa utaenda kuondoa malalamiko yote ya vijana wa ulinzi shirikishi ya kutopata posho zao.
Amesema " sasa hivi kila Mwenyekiti wa shina atashirikiana na kiongozi wa Ulinzi shirikishi ili kukusanya michango katika kaya zinazopatikana katika shina husika ili kuwezesha ufanisi katika ukusanyaji wa michango hiyo ambayo ikikusanywa kikamilifu itawezesha kulipa posho, kununua sare, radio call, kulipia bima za afya".
Kwa upande wa mwakilishi kutoka uongozi wa ulinzi shirikishi katika wilaya ya Kipolisi Ukonga MG. 43790 Peter Charles ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa kwa lengo la kuongeza ufanisi na uwaminifu katika jamii.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wakaguzi kata 14 na vijana wa ulinzi shirikishi wapatao 200 ambao wametokea katika kata 14 zinazopatikana katika Wilaya ya Kipolisi Ukonga.
Social Plugin