James Makungu Sombi enzi za uhai wake akizungumza na Malunde 1 blog nyumbani kwake Kisesa Mwanza
*****
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Manju maarufu na Mtaalamu wa Masuala ya Utamaduni wa Kabila la Kisukuma James Sombi (89) amefariki dunia.
James Sombi ni miongoni mwa waanzilishi wa Makumbusho ya Kabila la Wasukuma Bujora Mwanza ambaye enzi za uhai wake alikuwa mcheza ngoma maarufu ya Bugobogobo na Zeze aliyetangaza utamaduni wa Kabila la Wasukuma ndani na nje ya Tanzania.
Kwa mujibu wa mtoto wake aitwaye Veronica aliyezungumza na Malunde 1 blog, amesema Mzee James Sombi amefariki dunia Jumatatu Februari 27,2023 saa nane mchana baada ya kuanguka.
"Mzee ametutoka baada ya kuanguka ghafla akiwa nyumbani kwake Kisesa Mwanza. Alikuwa anasumbuliwa na tatizo kwenye mishipa ya moyo na alikuwa anasema kifua kinauma na ghafla mchana akaanguka", ameeleza Veronica.
"Mwili wake umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ,utaagwa kwenye makumbusho ya Bujora kisha utaletwa hapa nyumbani Kisesa na mazishi yatafanyika siku ya Jumamosi Machi 4,2023 katika kijiji cha Mwamanga Magu kama alivyotaka yeye kabla ya kifo chake na kwa kuwa enzi za uhai wake alikuwa mcheza ngoma pia atachezewa ngoma ya kimila wakati wa kuaga mwili wake na siku ya mazishi yake",amesema Veronica.
James Makungu Sombi alizaliwa mwaka 1934 katika kijiji cha Mwamanga wilayani Magu mkoani Mwanza.
Enzi za uhai wake, James Sombi alishirikiana na aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Bujora, Padri Daud Clementi, (RIP) walianzisha kituo cha utamaduni cha Bujora na kukifanya kuwa moja ya vituo vya utalii maarufu Kanda ya Ziwa.
Walikusanya kila aina ya mti uliopatikana katika himaya ya wasukuma na kupanda mahali hapo, viumbe wengine kama nyoka, fisi, Simba, chui, nk. wakakusanya vifaa mbalimbali vilivyotumiwa na watemi wa Kisukuma, ngoma na silaha za jadi.
Chini ya uongozi wake, kituo cha Bujora kilitoa mafunzo ya utamaduni na wageni wengi walifika kujifunza lugha ya Kiswahili na Kisukuma pamoja na kucheza ngoma za Kisukuma na michezo ya bao, mieleka n.k.
James Makungu Sombi akitoa burudani enzi za uhai wake
Soma pia
JAMES SOMBI : KUFANYA SANA MAPENZI KUNAPUNGUZA SIKU ZA KUISHI
MZEE SOMBI : VIJANA WANAOGOPA KUOA KWA SABABU HAWANA KAZI....HAWATAKI USUMBUFU
BABU ATOA DAWA YA KUKOMESHA UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME...VIBAMIA