Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa(IRUWASA) Mhandisi David Pallangyo akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo katika ukumbi wa Habari -MAELEZO.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa(IRUWASA) Mhandisi David Pallangyo akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo katika ukumbi wa Habari -MAELEZO.
Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 Blog-DODOMA
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) imevuka lengo la sera ya Maji na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kutoa huduma ya usambazaji maji kwa mji wa Iringa na maeneo ya pembezoni inayowafikia wakazi hao kwa asilimia 97.
Aidha imefanikiwa kupunguza kiasi cha maji yasiyolipiwa (NRW) kwa upande wa Iringa Mjini kutoka wastani wa 24.6 (2020) hadi wastani wa 22.52% (mwezi Desemba, 2022) ambapo idadi ya wateja/maunganisho ya Majisafi imeongezeka kutoka 28,133 (2020) hadi 40,549
(Desemba, 2022).
Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Mhandisi David Pallangyo ameeleza hayo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya IRUWASA na kueleza kuwa katika eneo la TEHAMA wamefanikiwa kwa kufunga mita za malipo ya kabla (prepaid water meters) kwa wateja 6,752 na kuwa Mamlaka inayoongoza nchini kwa kufunga mita nyingi za maji za malipo kabla.
Kutokana na hayo wamefanikiwa kuhakikisha huduma ya maji Mjini Iringa na maeneo ya pembezoni inapatikana kwa wastani wa saa 23 kwa siku na kuongeza ukusanyaji maduhuli (revenue collection) kwa huduma zilizotolewa kutoka wastani Tshs 770M/= (2020) kwa mwezi hadi 860M/= (2023) na kwamba hali hiyo imeiwezesha mamlaka hiyo kuweza kugharamia kwa kiasi kikubwa uendeshaji wa Taasisi.
Akizungumzia usambazaji wa Majisafi, Mhandisi huyo amesema shughuli mbalimbali za usambazaji majisafi hufanywa kwa kutumia miundombinu ya mtandao wa mabomba, vituo vya kusukuma maji na matenki ya kuhifadhia maji.
"Mtandao wa kusafirishia na kusambazia majisafi kwa Manispaa ya Iringa, maeneo ya pembezoni na Miji ya Ilula na Kilolo ina jumla ya urefu wa kilomita zipatazo 860,Mtandao huu unajumuisha matenki makubwa na madogo yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya meta za ujazo 8,735M3)ambapo miundombinu hii pia inajumuisha jumla ya vituo vya kusukumia maji tisa ,"amesema.
Amesema,kupitia miundombinu hiyo ya usambazaji majisafi, huduma majisafi mewafikia asilimia 97 ya wakazi wote wa Manispaa ya Iringa na maeneo ya pembezoni yanayohudumiwa na IRUWASA huku muda wa upatikanaji wa maji ukiwa wastani wa saa 23.
Kwa upande wa Mji wa Kilolo amesema huduma ya maji imewafikia asilimia 85 ya wakazi ambao hupata huduma ya maji kwa wastani wa saa 18 wakati kwa upande wa Mji wa Ilula huduma ya maji imewafikia asilimia 72 ya wakaazi ambapo upatikanaji wa maji ni wastani wa saa 18 kwa siku.
"Hadi kufikia 31 Desemba, 2022, IRUWASA ilikuwa na jumla ya maunganisho (wateja) 40,549,kiwango cha upotevu wa maji (NRW) kwa upande wa Manispaa ya Iringa ni wastani wa asilimia 22.5 wakati kwa Miji ya Kilolo na Ilula imeshuka kutoka asilimia 80 (wakati inakabidhiwa IRUWASA 2020) hadi wastani wa asilimia 40 (Desemba, 2022),"amesema
Social Plugin