Na Dotto Kwilasa,Malunde 1Blog, DODOMA.
BODI ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu imewataka wadau wa maji nchini kuzingatia na kufuata taratibu za uchimbaji wa visima vya maji ikiwemo kupata vibali halali ili kupata maji yenye ubora na kuondokana na malalamiko mengi ya maji yasiyo na viwango.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasi ameeleza hayo leo,Februari 7,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji chini ya bodi hiyo.
Amesema,wadau wa maji wanapaswa kufahamu madhara ya kuchimba visima bila vibali na kupelekea changamoto ya ubora wa maji kwenye maeneo mengi jambo linaloweza kuleta madhara kiafya.
Kutokana na hayo ameeleza baadhi ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kutumia maji yasiyo na madhara kuwa ni pamoja na kuhakikisha maji yanayopatikana baada ya kuchimbwa yanapelekwa maabara kuchunguzwa iwapo yanafaa kwa matumizi au lah.
Sambamba na hayo amesema kuwa bodi hiyo imejipanga kuhakikisha inamaliza changamoto ya tatizo la maji katika mikoa ya Dar es salaam,Pwani na Morogoro kwa kuchimba visima kumi vyenye maji ya kutosha.
Bodi hiyo pia imejipanga kuhakikisha inatatuza tatizo la maji katika mikoa ambayo imekuwa na changamoto ya maji hususani katika mkoa wa Pwani, Morogoro na Dar es salaam.
"Bodi ya maji imeweza kufanikiwa kubaini vyanzo vipya vya maji ambavyo ni eneo la Nzuguni lililopo Jijini Dodoma kwa kuwa lina maji ya kutosha na hivi karibuni tutatangaza katika gazeti la serikali kuwa ni benki ya maji pamoja na Dakawa katika mji wa Dodoma,"amesema.
Kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji amesema wanahakikisha vyanzo vyote vinatunzwa kwa ajili ya kutunza maji yaliyopo chini ya Ardhi huku akiwataka watanzania kuepukana na tabia ya uchimbaji ovyo wa visima vya maji kwa maelezo kuwa kunaweza kusababisha kuchafua maji yaliyopo chini ya ardhi jambo ambalo ni hatari kuweza kuondoa sumu ambayo inaweza kujitokeza.
Amesema mikakati ya Bodi hiyo ni kulifanya Bonde hilo kuwa lenye Mazingira safi na kijani linalotunza na kuendeleza vyanzo vya maji kwa maendeleo ya Binadamu kijamii na kiuchumi yanayostahimili majanga yanayoweza kutona na maji.
Social Plugin