Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog-DODOMA.
BODI ya Usimamizi wa Stakabadhi ghalani (WRRB) imeeleza kuchukizwa kwake na madalali wanao warubuni wakulima kwa kutumia mbinu za kwenda mashambani na kuwadalalia mazao
yao kwa bei ya chini kitu ambacho kinaendelea kudidimiza maendeleo ya wakulima .
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo (WRRB)Asangye Bangu ameeleza hayo leo Februali 15,2023 wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo na kuwataka madalali kuacha tabia hiyo na badala yake kuwaacha wakulima waingie kwenye mfumo wa Stakabadhi ghalani ili kuuza mazao yao kulingana na bei iliyopo sokoni.
Amesema kumekuwa na wimbi la watu wanaokwenda mashambani kwa wakulima wenye hali ya chini na kununua mazao wa bei ya chini jambo ambalo linamdidimiza mkulima kwa kuwa anatumia nguvu nyingi kulima bila kupata faida inayoendana na nguvu aliyopoteza.
"Sisi kama WRRB tunawapenda sana madalali, lakini niwaombe iwe mwisho kuwarubuni wakulima,acheni kuwafuata fuata na kuwaeleza habari ambazo siyo za kweli kwa manufaa yenu,acheni kuwanyanyasa wakulima,"amesema
Amesema kuwa wao kama WRRB wapo tayari na milango yao ipo wazi ili waweze kukaa pamoja na kujadiliana ni namna gani na wao watawaingiza katika Mfumo ili waendelee kunufaika badala ya kuuangalia mfumo kama changamoto.
"Natoa wito kwa madalali waache kuwarubuni wakulima wawaache wajiunge katika Mfumo wa Stakabadhi ghalani ili waweze kuuza mazao yao kwa bei ya ushindani iliyopo sokoni kwa kuendelea kuuza mazao shambani inaendelea kuwadidimiza wakulima kwa sababu madalali wengi wananunua mazao kwa bei ya chini tofauti kabisa na bei iliyopo kwenye mfumo,"amesema Bangu
Akieleza mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za ghalani amesema kuwa ni pamoja na ongezeko la bei za mazao, mapato ya mkulima na mapato ya Serikali kwa wastani wa asilimia 200% kutokana na urasimishaji, ongezeko la uzalishaji wa mazao kwa wastani wa asilimia 12% kwa mwaka na kichecheo cha ubora wa mazao yanayofikishwa sokoni.
"Mafanikio mengine ni upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao yanayopita kwenye mfumo wa stakabadhi za ghala, ongezeko la mapato ya uhakika kwa Serikali kuu na Serikali za mitaa na kukuza huduma za fedha vijijini,kufanikisha uanzishaji wa Soko la bidhaa Tanzania,"amesema na kuongeza;
Tangu kuanzishwa kwa Mfumo 2007/08 hadi 2020/21 ukuaji wa uzalishaji umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa 12% kwa mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa 2% kwa mwaka kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa stakabadhi za ghala kwa mfano katika zao la Korosho mara baada ya kuanzishwa kwa Mfumo palikuwa na ongezeko la asilimia 164% la bei kutoka Ths 350.00 msimu wa 2006/07,"amesisitiza
Aidha katika miaka minane tokea kuanzishwa kwa Mfumo 2007/08 hadi 2014/15 wastani wa ongezeko la bei kwa mwaka ulikuwa 25% kulinganisha na ongezeko la bei miaka minane kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo la 12% kwa mwaka kaunzia mwaka 1998/99 hadi 2006/07.
Social Plugin