Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DHAMANA ZA ZABUNI NA UTEKELEZAJI WA MIKATABA



***************************

Na Zawadi Msalla- PPRA

Kuna msemo usemao mipango siyo matumizi, na sababu kubwa ya watu kusema maneno hayo ni kutokana na vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katikati ya mpango ulio uweka hivyo kupelekea mpango huo kutokutimia au kuchelewa kutimia.

Vihatarishi katika michakato ya ununuzi ni moja ya kikwazo kikubwa katika kufikia azma ya kupata huduma bora katika ununuzi. Vihatarishi vinavyojitokeza katika michakato ya ununuzi hupelekea Malengo ya taasisi nunuzi kuharibika au kuchelewa.

Moja ya kihatarishi kikubwa katika mchakato mzima wa ununuzi wa Umma ni matendo ya wazabuni kujitoa kwenye mchakato wa zabuni na kutotekeleza mkataba wa ununuzi. Hali hii hupelekea taasisi nunuzi kutofikia malengo yake ya kupata bidhaa, huduma na kazi za ujenzi kwa wakati, kwa ubora na kwa gharama nafuu.

Katika kukabiliana na kihatarishi hicho miongozo mbalimbali imewekwa ikiwemo utaratibu wa kudai dhamana za zabuni na utekelezaji wa mikataba ambapo taasisi nunuzi huweka utaratibu wa kudai wazabuni kuwasilisha dhamana za zabuni na utekelezaji wa mikataba..

Dhamana ni kitu cha thamani au tamko linalotoa hakikisho kwa mpokea dhamana kwa ajili ya utatekelezaji wa wajibu fulani kwa mujibu wa makubaliano ili kuepusha kutokea kwa mambo yasiyotakiwa.

Mhandisi. Amini Mcharo ni mkurugenzi wa Idara ya kujenga uwezo na huduma za ushauri kutoka Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma(PPRA) anasema Kudai dhamana ni moja ya njia inayotumiwa na taasisi nunuzi Ili kudhibiti hatari ya kutofikia malengo yao kutokana na matendo ya wazabuni.

“Taasisi nunuzi hudai dhamana kutoka kwa wazabuni ili kujihakikishia kuwa wazabuni hawatajitoa katika michakato ya zabuni kabla ya wakati unaoruhusiwa, watakubali marekebisho ya bei zao, watakubali tuzo za zabuni na kutekeleza mikataba ya ununuzi kwa uaminifu” Mhandisi Mcharo anaelezea.

Dhamana hudaiwa kwa wazabuni katika hatua ya mchakato wa zabuni na usimamizi wa mkataba; dhamana zinazodaiwa wakati wa mchakato wa zabuni huitwa dhamana za zabuni na zile zinazodaiwa wakati wa usimamizi wa mkataba huitwa dhamana za utekelezaji wa mkataba.

Akielezea lengo la kudai dhamana ya zabuni Mhandisi Mcharo anasema ni kuhakikisha kuwa mzabuni yoyote aliyeomba zabuni husika, hataondoa zabuni yake kabla ya tuzo ya zabuni kutolewa kwa mzabuni mshindi au kuisha muda wa uhai wa zabuni yake. Pia, atakubali marekebisho sahihi ya mahesabu ya bei yake kama yalivyofanywa na taasisi nunuzi na atakubali tuzo ya zabuni kama itatolewa kwake iwapo atakuwa ndiye mzabuni mshindi.

Dhamana za utekelezaji wa mkataba pia zimelenga kuhakikisha kuwa mzabuni mshindi atatekeleza wajibu wake wa kusambaza bidhaa, kutoa huduma au kufanya kazi za ujenzi kama ulivyoanishwa kwenye mkataba wa ununuzi.

Iwapo mzabuni hatotekeleza mambo ambayo alitoa hakikisho la kuyafanya kwa mujibu wa dhamana aliyoitoa basi huchukuliwa hatua ikiwemo kufungiwa kushiriki michakato ya zabuni ya taasisi zote nchini au kutaifishwa kwa dhamana iliyowasilishwa.

Pia, akielezea kuhusu aina za dhamana zinazoruhusiwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma mtaalamu wa ununuzi kutoka PPRA Bw. Frank Yesaya anasema dhamana hizo zimegawanyika katika makundi makubwa mawili, moja ni dhamana ambazo zipo katika mfumo wa kifedha na mbili dhamana ambazo zipo katika mfumo wa tamko.

Bw. Yesaya anaeleza kuwa dhamana za mfumo wa kifedha ni pamoja na dhamana zinazotolewa na benki na mashirika ya bima; wakati dhamana za mfumo wa tamko zinahusisha mzabuni kujaza tamko sanifu lililopo kwenye nyaraka za zabuni husika ili kutoa hakikisho kwa taasisi nunuzi.

“Ni muhimu taasisi nunuzi kuthibitisha uhalali wa dhamana za mfumo wa kifedha zinazowasilishwa na wazabuni kutoka benki au mashirika ya bima yanayotoa dhamana husika” Alisema Bw. Yesaya.

Aidha, akielezea endapo mzabuni ataenda kinyume na dhamana aliyoiweka mtaalam huyo wa masuala ya Ununuzi Bw. Yesaya anaeleza kuwa iwapo mzabuni atakwenda kinyume na dhamana ya mfumo wa kifedha taasisi nunuzi wanayohaki ya kuitaifisha dhamana husika, na kueleza Zaidi kuwa endapo mzabuni akienda kinyume na dhamana ya mfumo wa tamko, taasisi nunuzi wanayohaki ya kuomba mzabuni afungiwe na PPRA ili asishiriki katika michakato ya taasisi nunuzi zingine kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili.

“Adhabu zinazotolewa kwa kukiuka masharti ya dhamana zimelenga kuhakikisha wazabuni wanakuwa makini katika utekelezaji wa zabuni zao”

Taasisi nunuzi wanaruhusiwa kuomba dhamana za mfumo wa kifedha iwapo thamani ya zabuni au mikataba ya ununuzi imefikia kiwango ambacho kinaruhusiwa kuomba dhamana za kifedha.

PPRA imetoa mwongozo wa dhamana unaotoa maelekezo kwa taasisi nunuzi kuhusu dhamana za zabuni na utekelezaji wa mikataba, kupitia mwongozo huo, imetambulishwa aina mpya ya dhamana ya utekelezaji wa mkataba ambayo ipo katika muundo wa tamko. Kwa kuanzia dhamana hii itadaiwa na taasisi nunuzi kwa mikataba ya ununuzi wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi isiyozidi fedha za kitanzania bilioni moja.

Wazabuni huingia gharama kupata dhamana za zabuni zilizo katika mfumo wa fedha, hivyo ni muhimu taasisi nunuzi kuomba dhamana hizo kwa zabuni ambazo zimefikia viwango vinavyoruhusiwa.

Taasisi nunuzi wanapoaihirisha michakato ya ununuzi huwaingiza wazabuni katika hasara ya kuendelea kukatwa marejesho ya dhamana za kifedha wakati michakato husika ilishafutwa.

Bila shaka wakati utafika dhamana za zabuni zilizo katika mfumo wa kifedha zitaweza kutolewa na benki na kuwasilishwa kwa taasisi nunuzi kupitia mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com